Habari MsetoSiasa

Ruto akejeliwa kupinga mabadiliko ya katiba

February 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

RUSHDIE OUDIA na BENSON AMADALA

VITA vya maneno kati ya Naibu Rais William Ruto na viongozi wa chama cha ODM kinachoongozwa na Raila Odinga, vilichacha Jumapili kuhusu kuandaliwa kwa kura ya maamuzi ili kubadilisha mfumo wa uongozi.

Dkt Ruto alisisitiza kuwa hataunga mkono jaribio lolote la kubadilisha katiba ili kuunda nafasi za uongozi kwa watu wachache, huku viongozi wa ODM nao wakimjibu kwa kusema kwamba mfumo wa uongozi unaojumuisha viongozi wote utahakikisha hata jamii ndogo zinawakilishwa serikalini.

“Mjadala kuhusu nani anafaa kushikilia wadhifa upi serikalini ulitamatishwa wakati wa uchaguzi wa 2017 Wakenya walipopigia kura Jubilee. La muhimu mno kwa walio serikalini na upinzani ni kuungana kwa ajili ya maendeleo,” akasema Dkt Ruto.

Akizungumza katika Kanisa Katoliki la Christ the King, Amalemba mjini Kakamega, Naibu Rais aliwaomba Wakenya kuwapuuza viongozi wa upinzani wanaoendeleza kampeni ya mapema kutaka marekebisho ya katiba yafanywe ili “kuwaundia vyeo serikalini”.

Hata hivyo, Kiongozi wa Wachache kwenye Bunge la Seneti, James Orengo na Waziri wa Ugatuzi, Eugene Wamalwa walipuuzilia mbali matamshi ya Dkt Ruto kwa kusema kwamba wakati umewadia wa nchi kuandaa kura ya maamuzi ili kuleta manufaa kwa wananchi.

Bw Orengo alimwambia Dkt Ruto akome “kuhubiri uongo” kuhusu kura ya maamuzi, na badala yake aelewe makubaliano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga yanacholenga, huku akisisitiza kwamba kamati iliyoundwa na wawili hao tasaidia kuleta umoja nchini.

“Ningependa kuwaambia wanaoshuku nia ya kuandaliwa kwa kura ya maamuzi kukoma kufanya hivyo. Naibu Rais anafaa kutumia muda wake kuelewa manufaa ambayo kura hiyo itawaletea wananchi. Mabadiko yaja hivi karibuni,” akasema Bw Orengo.