Habari Mseto

Ruto azuru makao makuu ya Jubilee

September 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na LEONARD ONYANGO

NAIBU Rais William Ruto alifanya ziara ya ghafla katika makao makuu ya chama cha Jubilee mtaani Pangani, Nairobi, jana Jumanne.

Dkt Ruto alikuwa ameandamana na Mbunge wa Lang’ata Nixon Korir ambapo alipata mapokezi kutoka kwa maafisa wa ngazi ya chini kwani Katibu Mkuu Raphael Tuju na Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe hawakuwepo.

Kulingana na Bw Denis Itumbi, mmoja wa maafisa wa mawasiliano wa kibinafsi wa Naibu wa Rais, Dkt Ruto alienda katika makao makuu ya Jubilee kupanga mikakati ya chaguzi ndogo zitakazofanyika Desemba 15, 2020.

Chaguzi hizo ni ubunge wa Msambweni na udiwani katika Wadi za Kahawa Wendani (Kiambu), Lake View (Nakuru), Kisumu Kaskazini (Kisumu), Wundayi/ Mbale (taita Taveta) na Dabaso (Kilifi).

Chama cha ODM tayari kimeidhinisha wawaniaji wawili, Omar Idd Boga na Nicholas Zani kushiriki katika kura za mchujo za chama hicho.

Kiti cha Msambweni kilisalia wazi kufuatia kifo cha Suleiman Dori aliyeaga dunia Machi mwaka huu.