• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Sababu ya Kalonzo kuingia safina ya UhuRaila

Sababu ya Kalonzo kuingia safina ya UhuRaila

Na LEONARD ONYANGO

SIASA za Kenya zilichukua mkondo mpya jana baada ya vyama vya Wiper na CCM kutangaza rasmi kuwa vitashirikiana na Jubilee.

Kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka na mwenzake wa CCM (Chama cha Mashinani), Bw Isaac Ruto walitia saini mkataba wa maelewano na Jubilee katika makao makuu ya chama hicho tawala -Pangani, Nairobi.

Kwa hatua hiyo, Bw Kalonzo na Ruto wanaungana rasmi na muungano wa Jubilee unaojumuisha pia Kanu inayosimamiwa na Seneta Gideon Moi.

Hata hivyo, hatua hiyo imeibua maswali mengi kuhusu iwapo Kenya inarejea katika enzi ya chama kimoKanu Kanu au la. Aidha, taswira nyingine inayojitokeza baada ya urasmishaji wa ushirikiano huo ni iwapo Rais Uhuru Kenyatta aliye kiongozi wa Jubilee amefaulu kumtenga naibu wake Dkt William Ruto kwa kuendelea kuwakaribisha mahasimu wa mwenzake chamani.

Mwezi jana, Rais aliamua kuunda muungano na Kanu.

Akitangaza uamuzi huo jana, Bw Musyoka alifichua kuwa janga la virusi vya corona lilitatiza mpango wa Wiper kujiondoa katika muungano wa NASA unaojumuisha ODM, Amani National Alliance (ANC), CCM na Ford Kenya.

“Leo tumetia saini mkataba wa ushirikiano na wala si kuunda muungano na Jubilee. Kwa sasa chama cha Wiper hakiwezi kufanya muungano na Jubilee kwani bado tuko ndani ya NASA,” akasema Bw Musyoka aliyekuwa akizungumza baada ya hafla ya kutia saini mkataba huo.

“Lakini tunatamani kufanya muungano wa kisiasa na Jubilee; baada ya janga la virusi vya corona, tutashauriana na wanachama ili waturuhusu kujiondoa katika muungano wa NASA tuingie kabisa ndani ya Jubilee,” akaongezea.

Bw Musyoka alisema kuwa Rais Kenyatta hakufika katika makao makuu ya Jubilee kushuhudia hafla ya kutia saini mkataba huo kama tahadhari baada ya watu wanne kupatikana na virusi vya corona kwenye Ikulu ya Nairobi.

Rais Kenyatta aliwakilishwa na Katibu Mkuu wa Jubilee, Bw Raphael Tuju, mwenyekiti Nelson Dzuya na naibu wake David Murathe.

Mkataba huo unamaanisha kwamba wabunge na maseneta wa chama cha Wiper sasa watasaidia Rais Kenyatta kusukuma ajenda yake ndani ya Bunge la Kitaifa na Seneti.

“Kadhalika, tutaunga mkono juhudi za Rais Kenyatta kutaka kuunganisha Wakenya wote kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) na vita dhidi ya ufisadi,” akasema Bw Musyoka aliyekuwa ameandamana na mwenyekiti wa Wiper, Bw Chirau Mwakwere, Katibu Mkuu Judith Sijeny na Seneta wa Makueni, Bw Mutula Kilonzo Junior.

Kulingana na Bw Kilonzo; Rais Kenyatta ndiye aliyeshawishi viongozi wa Wiper kushirikiana na Jubilee.

“Hafla ya leo ni ishara kwamba tumekubali wito wa Rais kututaka kufanya kazi naye. Tumekaribishwa vizuri Jubilee. Tumetia mkataba wa maelewano ili kusiwe na utata baadaye,” akasema Seneta Kilonzo.

Kiongozi wa CCM, Bw Ruto alisema kuwa aliamua kushirikiana na Jubilee kwa ajili ya amani.

“Tumeamua kushirikiana na Jubilee kwa sababu Rais Kenyatta ana ajenda nzuri ya kuunganisha Wakenya. Sisi ni wapenda amani,” akasema.

Katibu Mkuu wa CCM Zedekiah Bundotich, almaarufu Buzeki, alifichua kuwa Rais Kenyatta alianza mazungumzo na gavana huyo wa zamani wa Bomet mara tu baada ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Rais Kenyatta sasa amefanikiwa kutia kibindoni vyama vinne vikuu; ODM, Kanu, Wiper na CCM huku kukiwa na ripoti kwamba kiongozi huyo wa nchi ananuia kufanyia mabadiliko baraza lake la mawaziri ili kuwezesha Bw Ruto na Bw Musyoka kupata nyadhifa serikalini.

Muungano huo umeongeza masaibu ya Naibu wa Rais Ruto ambaye ametengwa na Rais Kenyatta.

Hatua hiyo pia inamaanisha kuwa upande wa ‘upinzani’ sasa umesalia na Naibu wa Rais Dkt Ruto, Bw Musalia Mudavadi wa ANC na Seneta Moses Wetangu wa Ford Kenya.

You can share this post!

Vilio watoto 4,000 wakipachikwa mimba Machakos

Serikali yaonya tiba ya corona isitumiwe ovyo

adminleo