Sababu ya Moi kubeba rungu kila alipoenda
Na WANDERI KAMAU
RUNGU maalum aliyobeba Rais Mstaafu Daniel Moi wakati wa utawala wake, itakuwa miongoni mwa vifaa vitakavyowekwa karibu naye, wananchi wanapoendelea kutazama mwili wake.
Rungu hiyo imetengenezwa kwa dhahabu na pembe ya ndovu.Itakuwa mara ya kwanza ambapo Wakenya wataona rungu hiyo kwa karibu.
Bw Moi aliibeba rungu hiyo kwa miaka 24 aliyoiongoza nchi.Rungu hiyo ilipewa msimbo wa ‘Fimbo ya Nyayo’ kama ishara ya mamlaka makubwa aliyokuwa nayo.Rungu daima ilibaki karibu na Bw Moi.
Kwa wakati mmoja, ilibidi rungu nyingine kusafirishwa kutoka Kenya hadi Australia kwa dharura, baada ya ile aliyokuwa nayo kuvunjika akiwa ziarani Amerika.
Kwenye mahojiano wakati mmoja, Katibu wa Kibinafsi wa Bw Moi Lee Njiru, alisema kuwa kiongozi huyo hakutosheka bila rungu hiyo katika hafla za umma.
“Mzee (Moi) hangeacha rungu hiyo, kwani ilikuwa kama mojawapo ya sehemu ya kuu ya utawala wake. Ni rungu aliyoithamini sana,” akasema.
Wakenya walilazimika kubuni nadharia mbalimbali kuhusu rungu hiyo, kwani Bw Moi hakuwahi kuzungumzia hadharani kuhusu maana yake.
Kifaa kingine maalum ambacho kitawekwa karibu na mwili wake, ni kiti maalum ambacho alikuwa akikalia kwenye hafla mbalimbali za umma.Kiti hicho kina nembo ya serikali, kuonyesha kuwa ndiye alikuwa mamlakani.
Inaelezwa kuwa lazima kiti hicho kingesafirishwa katika kila hafla ambayo angelazimika kuketi.Na ikizingatiwa kwamba alikuwa Mkristo, vile vile kutakuwepo na Biblia kuonyeasha imani yake.
Katika utawala wake wote, hakukosa kuhudhuria hafla ya ibada kanisani kila Jumapili. Alikuwa mshirika wa kanisa la African Inland Church (AIC).
Kando na hayo, maua maalum yatawekwa kando na mwili wake, ikizingatiwa kuwa alipenda kuweka maua kwenye mfuko wa mbele wa suti alizovaa.
Bw Moi alifariki Jumanne katika Nairobi Hospital, akipokea matibabu baada ya kuugua kwa muda mrefu. Atazikwa Jumatano nyumbani kwake katika eneo la Kabarak.