• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Sababu za ODM kuiponda hatua ya maafisa wa KRA, KPLC kupewa kazi chamani UDA

Sababu za ODM kuiponda hatua ya maafisa wa KRA, KPLC kupewa kazi chamani UDA

NA WANDERI KAMAU

CHAMA cha ODM kimemtaka mwenyekiti wa Bodi ya Halmashauri ya Kukusanya Ushuru Kenya (KRA), Bw Anthony Mwaura, kujiuzulu kutoka nafasi hiyo, baada ya kuteuliwa kama mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEB) ya UDA.

Bw Mwaura aliteuliwa kuongoza bodi hiyo, kwenye mageuzi ya uongozi wa chama hicho yaliyotangazwa Jumanne, kinapojitayarisha kufanya chaguzi zake za mashinani baadaye mwezi huu.

Kando na Bw Mwaura, UDA ilimteua mwenyekiti wa bodi ya Kampuni ya Umeme Kenya (KP), kama mkuu wa Kitengo cha Kutatua Mizozo.

Kwenye kikao na wanahabari Jumatano baada ya kikao cha Kamati Kuu ya Uratibu wa Chama (CMC), Nairobi, ODM ilisema kuwa, Bw Mwaura na viongozi wengine hawafai kushikilia nyadhifa za kisiasa na za serikali kwa wakati mmoja.

“Huku ni sawa na kuturejesha katika miaka ya 1980 ambapo maafisa wa serikali walikuwa wakitumika kuendeleza maslahi ya kisiasa ya chama kilicho uongozini. Lazima Bw Mwaura ajiuzulu na kuhudumu katika nafasi moja,” akasema Katibu Mkuu wa ODM, Bw Edwin Sifuna, kwenye taarifa aliyosoma kwa niaba ya viongozi wa chama hicho.

ODM pia iliilaumu serikali kutokana na hatua yake kujikokota kwenye utatuzi wa mgomo wa madaktari unaondelea nchini.

Chama hicho pia kiliikemea serikali kutokana na kuchelewa kwa ufadhili wa shule, sakata ya mbolea ghushi nchini, ucheleweshaji wa utekelezaji wa Ripoti ya Kamati ya Mazungumzo ya Kitaifa (NADCO) na ucheleweshaji wa ufadhili wa vyama vya kisiasa.

“Tumehofishwa na mtindo wa kipuuzi ambao serikali imechukua katika kutatua mgomo wa madaktari na athari ambazo umekuwa nazo kwa Wakenya. Serikali inaonekana kutojitolea na kuwa na uwezo wa kutatua mgomo huo,” akasema BW Sifuna.

Kinara wa chama, Bw Raila Odinga, pia alikuwepo. Wengine waliokuwepo ni Naibu Kiongozi wa Chama, Bw Wycliffe Oparanya, mwenyekiti wa kitaifa wa chama, Bw John Mbadi, Kiranja wa Wachache Junet Mohamed kati ya viongozi wengine.

  • Tags

You can share this post!

Serikali yachukua maelezo kimya kimya ya wakulima...

Mateso mpaka lini? Sh2.4 bilioni zakosa kuridhisha...

T L