• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
Sababu za upinzani mkali kwa hatua ya kupokonya basari wanafunzi 700 waliofeli masomoni

Sababu za upinzani mkali kwa hatua ya kupokonya basari wanafunzi 700 waliofeli masomoni

NA KALUME KAZUNGU

HATUA ya serikali ya Kaunti ya Lamu ya kuwatema wanafunzi karibu 700 kutoka kwa mpango wake wa ufadhili wa karo ya shule za sekondari kutokana na kufeli kwao masomoni imepingwa vikali na baadhi ya viongozi na wakazi, ikiwemo wazazi eneo hilo.

Serikali ya kaunti ya Lamu, ikiongozwa na Gavana, Issa Timamy awali ilikuwa imetoa onyo kwa wanafunzi wanaofadhiliwa kupitia basari ya kaunti kufanya bidii masomoni la sivyo watapokonywa ufadhili huo na jukumu la kuwasomesha liachiwe wazazi wao.

Mwaka huu, baada ya muhula kuanza, serikali ya kaunti ilitekeleza uchunguzi wa maendeleo ya wanafunzi inaowafadhili kupitia matokeo ya mitihani waliyofanya kwenye shule mbalimbali za upili, ambapo wote waliopatikana wakiandikisha alama isiyoridhisha, ikiwemo C- kwenda chini walifyekwa kutoka kwa orodha ya watakaoendelea kufaidi ufadhili huo wa karo kutoka kwa kaunti.

Wakizungumza kwenye shule ya msingi ya wavulana ya Lamu kisiwani Lamu Jumamosi wakati wa kongamano la elimu lililojumuisha kuwapokeza zawadi wanafunzi bora, viongozi na wananchi walisema hairidhishi kuwatema wanafunzi kutoka kwa ufadhili huo kwa kigezo cha kuanguka mitihani kwenye shule zao.

Wakiongozwa na Seneta Maalumu, Bi Shakila Abdalla, walichacha kuwa kuondolewa kwa wanafunzi kwenye ufadhili wa karo ya kaunti huenda kukawasukuma wengine kujiingiza kwenye mihadarati, ngono, mimba na ndoa za mapema.

Bi Abdalla alikosoa hatua hiyo ya kaunti, akisema iko kinyume kabisa na katiba ya nchi inayosisitiza haja ya watoto kuwa na haki ya kusoma na kuendelezwa kielimu maishani.

“Kamwe siridhishwi na hatua ya utawala wako Gavana wa kuwatema wanafunzi wasiopungua 700 kutoka kwa ufadhili karo ya sekondari eti kwa kigezo cha kuanguka mitihanini. Hawa wanafunzi waliotemwa hatima yao ya elimu itakuwaje ikizingatiwa kuwa wanatoka familia zisizojiweza? Hofu yangu ni kwamba wengi wa hao wanafunzi waliotemwa, hasa wasichana, huenda wakaishia kudanganywa, kupachikwa mimba mitaani na hata kuolewa mapema bila ya kuafikia ndoto yao ya elimu,” akasema Bi Abdalla.

Kiongozi huyo alimsihi Gavana Timamy kulizingatia upya suala hilo kwa kuhakikisha wanafunzi wote 700 wamerudishwa kwenye orodha ya wanaofaa kufadhiliwa na kaunti.

“Kwanza nakushukuru Gavana wetu, Issa Timamy, kwa kuibuka na mpango wa kufadhili wanafunzi werevu na wenye uhitaji kwenye jamii zetu. Ila zingatia hawa wanafunzi 700 mliowaondoa kutoka kwa ufadhili wa basari ya kaunti. Ningeomba warudishwe ili na wao waafikia ndoto yao ya elimu,” akasema Bi Abdalla.

Kauli yake iliungwa mkono na baadhi ya wazazi waliohojiwa na Taifa Leo ambao walitaja kutemwa kwa wanafunzi hao 700 kuwa dhuluma.

Kiwango cha kupita werevu wao

“Ni kweli wanafunzi ni werevu na huenda mitihani waliyopewa shuleni ilikuwa ya kiwango cha kupiku werevu wao. Kuna wale ambao hata huteleza mitihanini, hivyo kuanguka na kisha kujitambua na kurejelea hali yao ya kawaida. Kwa nini kuchukua hatua ya haraka ya kuwaondoa kutoka kwa ufadhili? Gavana alifikiria upya jambo hilo kwani limewapa wazazi wengi, hasa wale wa familia maskini msongo wa mawazo,” akasema Bi Aisha Yusuf.

Bw Simon Kamau alisisitiza haja ya kuwepo kwa uvumilivu na huruma upande wa kaunti wakati inapofadhili wanafunzi badala ya kuwawekea vikwazo visivyofaa.

“Mara tunaambiwa mwanafunzi kupata basari ya kaunti lazima awe amefikisha alama 250 au 300 kwenye mtihani wa darasa la nane (KCPE). Je kwa wale ambao hawakufikisha alama hizo na wanatoka jamii zisizojiweza wafanyeje? Isitoshe, bado tuko na wanafunzi wengi waliofikisha alama hizo na hawakuzingatiwa katika ufadhili wa karo na hiyo hiyo kaunti. Tumechoka na hivi vikwazo visivyofaa kwa watoto wetu,” akasema Bw Kamau.

Kauli ya viongozi na wananchi hao inajiri wakati ambapo mwezi huu serikali ya kaunti, chini ya uongozi wa Gavana Issa Timamy, ilizindua mpango wa basari ya kima cha Sh11 milioni kuwasaidia wanafunzi werevu na wenye uhitaji kaunti ndogo ya Lamu Magharibi.

Zaidi ya wanafunzi 1000 walilengwa kunufaika na mgao huo.
Kwa upande wake, Bw Timamy alishikilia kuwa msimamo wa kaunti ni kuhakikisha kuna uwajibikaji miongoni mwa wanafunzi na wazazi waanaonufaika na mpango huo wa ufadhili wa basari.

Bw Timamy alisema kaunti haiku tayari kufadhili masomo ya wanafunzi ambao wenyewe hawana nia ya kusoma.

Aliweka wazi kuwa ikiwa mwanafunzi hafanyi vyema masomoni ataachiwa mzazi kuubeba mzigo wa kumlipia karo mwanawe.

“Mwanafunzi asiyewajibikia kusoma si mzigo wetu. Tutamwachia mzazi mzigo huo kuubeba mwenyewe. Lazima wanafunzi wafanye vyema masomoni ili waendelee kufaidi basari ya kaunti. Hilo litasaidia kuhakikisha kuna ushindani mkali, hivyo kuinua hata kiwango cha masomo eneo hili,” akasema Bw Timamy.
Mwisho

  • Tags

You can share this post!

Vilio vyashamiri kuhusu gharama ya stima nchini

Kila mara nahisi mkojo hauishi kwenye mrija!

T L