• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
SADFA: Ezekiel Mutua asimulia kuugua kwa babake huku naye akisubiri upasuaji

SADFA: Ezekiel Mutua asimulia kuugua kwa babake huku naye akisubiri upasuaji

NA MARY WANGARI

Mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Filamu Nchini (KFCB) Ezekiel Mutua amevutia hisia baada ya kusimulia jinsi ugonjwa wa babake ulivyomsaidia kuepuka upasuaji hatari wa moyo huku imani ya Wakenya katika madaktari nchini ikizidi kufifia.

Katika ujumbe aliochapisha Facebook mnamo Jumatano Dkt Mutua alieleza namna alivyopokea ujumbe wa dharura kuhusu hali ya afya ya babake mashambani wakati alipokuwa akikabiliana na ripoti mbaya kuhusu maradhi yake binafsi ya moyo.

“Nilipokea simu kwamba baba yangu alikuwa katika hali mbaya. Anaongea peke yake, anashindwa kudhibiti haja ndogo, na ameshindwa kusimama na kuanguka mara mbili,” alisema.

“Hizo zilikuwa habari za kuumiza na kutisha. Nilijua sikuwa mzima kiafya na nilipaswa kumwona babangu lakini hali ya babangu ilisikika kuwa mbaya zaidi. Ni lazima ningeshughulikia apate matibabu kwa dharura,” alisema.

Alipoenda hospitalini na kuelezwa kiwango chake cha shinikizo la damu kilikuwa juu kupindukia, alihusisha hali hiyo na habari mbaya alizopokea kumhusu babake. Japo kundi la madaktari lililokuwa likimhudumia lilimtaka alazwwe hospitalini na kufanyiwa upasuaji mawazo yake yalikuwa kwa babake.

“Fikra zangu zilimwendea babangu na kile ambacho kingetendeka endapo singekuwa na uwezo wa kumhudumia. Kulingana na jinsi madaktari walikuwa wakinihudumia, nilipangiwa kufanyiwa upasuaji pengine ulaya.

“Mawazo yangu yalimwendea baba yangu aliyekonga na hisia ya dharura ikanishinikiza kumtafutia matibabu. Nilihisi nilitaji kuwa mwenye nguvu na kuwepo kwa sababu yake,” anasema.

Hatahivyo, juhudi za Mutua za kuwashawishi matabibu waliokuwa wakimhudumia kumruhusu amshughulikie babake kwanza ziligonga mwamba huku wakisisitiza alihitaji matibabu ya dharura ya moyo.

“Kwa hakika kasi niliyokuwa nikishinikizwa kulazwa hospitalini na jinsi shughuli yote hiyo ilivyokuwa ikiendeshwa kwa njia isiyokuwa ya kitaaluma ilikera.”

Ni hapo alipoamua kumshughulikia babake kwanza na kukataa kulazwa akihofia habari hizo zingezorotesha hata zaidi afya ya babake. Alishirikisha usaidizi wa madaktari wa Nairobi na Machakos kumsafirisha babake kutoka mashambani ili kufanyiwa ukaguzi wa kimatibabu.

Baada ya matokeo madaktari walipendekeza kwamba babake alihitaji upasuaji wa haraka.

“Nilisisitiza kwamba hatupaswi kumkimbiza mzee wa miaka 100 kufanyiwa upasuaji. Nililazimika kumtafutia matibabu mbadala. Hatimaye mwenzangu Japheth Kassanga aliniunganisha na Dkt Aideed Kahie ambaye kando na kumtibu babangu aliniunganisha na mtaalamu wa maradhi ya moyo anayenihudumia,” akasema.

Babangu sasa ni mzima kabisa, kumbukumbu yake iko shwari na hakuna anayeweza kusema alikuwa mgonjwa mahututi wiki iliyopita. Isingekuwa ni hali yake, ningekubali kirahisi kulazwa wiki jana na ni Mung utu anayejua ambacho ningekuwa napitia sasa,” alisema

Kisa cha Mutua ni mojawapo tu wa misururu ya visa ambapo Wakenya hujipata wakifanyiwa upasuaji kiholela na hata kupata matatizo ya kiafya baadaye. Hali hii imewafanya baadhi ya wananchi kukosa Imani na madaktari nchini wakiamua badala yake kutafuta tiba mbadala.

You can share this post!

Benki ya Dunia yamwaga mamilioni Nakuru kufadhili kilimo

ANN MWAI: Tajriba ya miaka 14 katika uigizaji

adminleo