Habari Mseto

Safari za ndege za kuingia na kutoka nchini kung’oa nanga Agosti 1

July 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

SHERIA na mikakati iliyotakiwa ili kuruhusu kurejelea safari za ndege kuingia ndani na kutoka nje ya nchi zimeafikiwa na kuidhinishwa na Wizara ya Afya.

Hii ni kufuatia agizo la Rais Uhuru Kenyatta mapema Julai 2020, ambapo alitangaza kwamba usafiri wa ndege kuingia ndani na kutoka nje ya Kenya utarejelewa mnamo Agosti 1, 2020, japo akaamuru idara husika kwa ushirikiano na Wizara ya Afya kuweka sheria na mikakati.

Safari za ndani kwa ndani nchini zilirejelewa Julai 15, miezi kadhaa baada ya kusimamishwa, kama njia mojawapo kuzuia kuenea kwa Covid-19.

Alhamisi, Waziri wa Uchukuzi James Macharia alitangaza kwamba mpangilio wa sheria na mikakati iliyotakiwa kuruhusu usafiri wa ndege kuingia ndani na kutoka nje, umekamilika na kuidhinishwa na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe.

“Mahitaji yote yamekamilika na kuidhinishwa na Waziri wa Afya,” akasema Bw Macharia, akihutubia wanahabari Afya House, Nairobi, na kuotoa mwelekeo wa safari za ndege kuingia ndani na kutoka nje ya nchi.

Mikakati iliyowekwa ni pamoja na kila abiria anayetua katika nyanja za ndege kutakiwa kuwa na cheti cha Covid-19, kinachoonyesha hana virusi vya corona.

Abiria watafanyiwa vipimo vya joto, na kiwango kinapaswa kuwa kisichopita nyuzijoto 37.5 kipimo cha sentigredi.

Waziri Macharia alisema wenye kikohozi kisichoisha, ugumu wa kupumua na kiwango cha juu cha joto lisilopungua, hawatakuwa na budi ila kupelekwa katika karantini ya lazima.

Abiria wanaotoka China, Korea Kusini, Japan, Canada, Zimbabwe, Ethiopia, Uswisi, Rwanda, Uganda, Namibia na Morocco, ndio wataruhusiwa kuingia nchini, Bw Macharia akisema mataifa hayo yamefanikisha jitihada katika kudhibiti msambao wa corona.

“Watakaofika baada ya saa za kafyu, lazima waonyeshe stakabadhi halali za safari zao za ndege ili waruhusiwe kuelekea katika mikahawa watakayolala au makwao. Madereva wa teksi au magari yatakayowabeba sharti yaonyeshe stakabadhi wametoka katika uwanja wa ndege,” akafafanua Waziri.

Kwa wanaopanga kusafiri nje ya nchi, wametakiwa kujua mahitaji ya mataifa wanayolenga kuzuru.

Waziri Macharia alisisitiza wahudumu wa ndege wahakikishe mikakati yote ya Wizara ya Afya imetekelezwa wakati wa safari, ikiwemo kuvalia maski na kuzingatia umbali kati ya mtu na mwenzake.