Safaricom ‘iliwekewa presha’ kuteua Mkenya
Na CHARLES WASONGA
KAIMU Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya mawasiliano ya Safaricom Michael Joseph ameungama bodi ya kampuni hiyo iliteua Mkenya kwa wadhifa huo kutokana na presha kutoka kwa serikali.
Akihojiwa Alhamisi usiku katika runinga ya moja nchini, Bw Joseph alisema bodi hiyo ilifikia uamuzi wa kumteua Peter Ndegwa baada ya uchunguzi wa takriban mwaka mmoja, humu nchini na mataifa ya nje.
“Tulipitia utaratibu mrefu katika juhudi zetu za kuteua Afisa Mkuu Mtendaji mpya. Tulitaka kuwa waangalifu kwa sababu serikali na wenye hisa walitaka mtu huyo awe Mkenya,” akasema.
“Mchakato huo ulichukua muda mrefu wa takriban mwaka mmoja. Hatimaye, tulishawishika kuwa Peter ndiye bora zaidi,” Bw Joseph akaongeza.
Alielezea imani kuwa Bw Ndegwa atatoa uongozi bora kwa Safaricom ikizingatiwa kuwa ana tajriba kubwa aliyopata katika kampuni nyingi za kimataifa zilizoandikisha ufanisi mkubwa.
“Amefanya kazi Nigeria, Ghana na Kenya. Wakati huu anafanya kazi katika kampuni kubwa kama Diageo na nina imani kwamba ni chaguo bora kwa kazi hiyo,” Bw Joseph akaeleza.
Alisema ni miaka 19 tangu kampuni ya Safaricom ilipoanzishwa na “hivyo ni jambo la busara ikiwa itaongozwa na Mkenya.”
Mnamo Aprili mwaka huu Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) Joe Mucheru alinukuliwa akipendekeza kuwa cheo cha Afisa Mkuu Mkuu Mtendaji wa Safaricom kinapaswa kushikiliwa na Mkenya baada ya muda wa kuhudumu wa marehemu Bob Collymore kukamilika.
“Hakuna kitu spesheli katika uendeshaji wa kampuni za mawasiliano, naamini Mkenya pia anaweza kuendesha Safaricom kama Afisa Mkuu Mkuu Mtendaji,” akasema wakati huo.
Serikali inamiliki asilimia 35 ya hisa katika Safaricom sawa na Vodacom kutoka Afrika Kusini huku kampuni ya Vodafone kutoka Uingereza ikimiliki asilimia tano ya hisa. Hisa zingine zinamilikiwa na watu binafsi.