Habari Mseto

Safaricom yanunulia wavuvi injini za boti

November 2nd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na Kalume Kazungu

SEKTA ya uvuvi kaunti ya Lamu, imepigwa jeki baada ya wakfu wa Safaricom kununua injini za boti kwa wavuvi eneo hilo zilizogharimu kima cha Sh 0.8 milioni.

Shughuli hiyo ilitekelezwa mjini Kizingitini, ambapo mashine hizo za boti zilikabidhiwa muungano wa kibinafsi wa wavuvi kwa jina Tawasal Fishermen Self-Help Group.

Kijiji cha Kizingitini ni mojawapo ya maeneo ambayo ni ngome kuu ya uvuvi Kaunti ya Lamu.

Takriban asilimia 97 ya wakazi wa Lamu Mashariki hutegemea uvuvi ili kujikimu maishani.

Sekta ya uvuvi eneo hilo aidha imekuwa na changamoto kufuatia utovu wa usalama unaochangiwa na magaidi wa Al-Shabaab hasa kwenye maeneo yanayopakana na Somalia, ikiwemo Kizingitini na Ishakani, Kaunti ndogo ya Lamu Mashariki.