• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 12:31 PM
Samboja na madiwani wake watakiwa kutafuta suluhu

Samboja na madiwani wake watakiwa kutafuta suluhu

Na LUCY MKANYIKA

HUKU Gavana Granton Samboja akiendelea kushikilia msimamo wake wa kuvunja serikali ya kaunti ya Taita Taveta, viongozi mbalimbali wanazidi kutoa ushauri wao wa kumtaka kukubali mazungumzo na madiwani wa wadi za kaunti hiyo.

Mbunge wa Taveta, Dkt Naomi Shaban amevunja kimya chake kuhusu mzozo huo na kuwataka viongozi hao kuusuluhisha. Mbunge huyo alisema ikiwa viongozi hao hawatasuluhisha malumbano baina yao, kaunti hiyo itasalia nyuma kimaendeleo.

“Ninawaomba gavana na madiwani wakae pamoja ili waokoe kaunti ya Taita Taveta,” akasema.

Alisema kuwa ana imani kuwa wazee, viongozi wa dini na wanasiasa wataungana ili kupatanisha pande hizo mbili. “Inawezakana watu kufanya kazi pamoja baada ya kutofautiana. Hata ndugu hukosana lakini hiyo haimaanishi kuwa hawawezi wakasuluhisha tofauti zao,” akasema.

Dkt Shaban alitofautiana na wabunge wenzake wa eneo hilo ambao wanaunga mkono mchakato wa kuvunjwa kwa kaunti hiyo.

Bw Jones Mlolwa (Voi), Andrew Mwadime (Mwatate) na Danson Mwashako (Wundanyi) wametangaza msimamo wao wa kumtaka Rais Uhuru Kenyatta kuvunja serikali hiyo ili wenyeji wachague viongozi wengine.

Seneta Jones Mwaruma vilevile alisema kuwa kuvunjwa kwa kaunti kutawapa fursa wenyeji kuwachagua viongozi wanaojali maendeleo.

Nao viongozi wa kidini katika kaunti hiyo wamemkosoa gavana na madiwani kwa kutafuta ushauri kwingine.

“Sisi tuko tayari kufanya majadiliano. Badala ya viongozi kutuhusisha wanasafiri nje ya nchi kutafuta ushauri, hilo si jambo la busara,” akasema kasisi Alice Mkombola wa chama cha makanisa katika kaunti hiyo.

You can share this post!

Kesi ya kupinga ‘Punguza Mizigo’ kuharakishwa

4 wanaswa na DCI kwa kuua mshukiwa wa wizi wa kuku

adminleo