Habari Mseto

Sampuli za kwanza zilipimiwa Afrika Kusini – Kagwe

September 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na SAMMY WAWERU

Tumepiga hatua kubwa mbele kama taifa katika vita na kampeni dhidi ya  virusi vya corona (Covid-19) tangu Kenya ilipothibitisha kuwa mwenyeji.

Waziri wa Afya, Mutahi Kagwe amesema taifa lilipoandikisha kisa cha kwanza cha ugonjwa huu ambao sasa ni janga la kimataifa, serikali haikuwa imejiandaa kikamilifu kuukabili.

Bw Kagwe alisema uhaba wa fedha na ukosefu wa vifaa maalum kufanya vipimo na kuzuia maambukizi ya corona, zilikuwa kati ya changamoto zilizohangaisha serikali.

Akizungumza katika kongamano la Covid-19 liloandaliwa katika ukumbi wa mikutano, KICC, Nairobi, Jumatatu, Waziri huyo wa afya alifichua kwamba sampuli za kwanza zilifanyiwa ukaguzi na vipimo Afrika Kusini kwa kile alitaja kama “Kenya kutokuwa na uwezo kufanya vipimo vya Covid-19”.

Aidha, alidokeza kwamba taifa halikuwa na maabara yoyote yenye uwezo kupima virusi vya corona, wakati huo. “Hakukuwa na maabara yoyote iliyokuwa na uwezo kupima Covid-19. Sampuli za kwanza zilifanyiwa vipimo nchini Afrika Kusini,” Bw Kagwe akaelezea.

Kupitia jitihada za serikali na kwa ushirikiano na wafadhili, Waziri alisema taifa lilifanikiwa kuimarisha mikakati kukabili corona.

Alisema mikakati kabambe iliyowekwa, Kenya imeweza kupiga hatua kubwa mbele katika vita na kampeni dhidi ya Covid-19.”Kwa sasa tuna jumla ya maabara 38 kote nchini ya kupima virusi vya corona. Ni rahisi kusahau tulikotoka na kutoridhia maendeleo tuliyofanya, ila ukweli ni kwamba tumepiga hatua mbele katika vita dhidi ya ugonjwa huu,” Waziri akasisitiza.

Kisa cha kwanza cha corona kilithibitishwa nchini mnamo Machi 13, 2020 na kulingana na Bw Kagwe taifa lilikuwa na vitanda 8 pekee maalum vya kulaza wagonjwa. Alisema kwa sasa kila kaunti ina zaidi ya vita 300.