• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:50 AM
Sarah Wairimu akanusha shtaka la kumuua mumewe

Sarah Wairimu akanusha shtaka la kumuua mumewe

Na Richard Munguti

SARAH Wairimu Kamotho Alhamisi alikanusha shtaka la kumuua mumewe Tob Cohen baada ya kukaa rumande kwa siku 38 upande wa mashtaka ukilumbana na wakili wake, Philip Murgor.

Na wakati huo huo, mshukiwa mwingine Peter Karanja alifikishwa mbele ya Jaji Stellah Mutuku akikabiliwa na shtaka la kumuua Cohen.

Kufikia sasa polisi wamewashtaki Bi Kamotho na Bw Karanja kwa mauaji ya mfanyabiashara huyo raia wa Uholanzi usiku wa Julai 19/20, 2019.

Bi Kamotho alisomewa shtaka la kumuua Cohen baada ya Jaji Mutuku kutupilia mbali ombi la kumzuia wakili Philip Murgor kumwakilisha katika kesi hiyo.

Mshtakiwa aliomba aachiliwe kwa dhamana lakini Kiongozi wa Mashtaka, Bi Catherine Mwaniki aliomba muda wa siku tano aandae orodha ya mashahidi watakaowekwa chini ya ulinzi wasivurugwe na mshtakiwa.

Mahakama ilikataa ombi hilo na kuamuru ombi la mshtakiwa la kuachiliwa kwa dhamana lisikizwe leo.

Kiongozi wa mashtaka na wakili wa familia ya Cohen, Bw Cliff Ombeta walikuwa wamedai kuwa Bw Murgor ni kiongozi wa mashtaka na hapaswi kumtetea mshukiwa huyo.

Lakini Bw Murgor alijitetea vikali akisema alijiuzulu Machi 7, 2019 kwa kumwandikia barua DPP na kurudisha faili ya kesi aliyokuwa amepewa kuongoza katika Mahakama ya Juu.

“Barua yangu ya kujiuzulu ilifika kwa afisi ya DPP Machi 7, 2019 pamoja na faili aliyokuwa amenipa. Nilipokea barua kutoka kwa Bi Catherine Muthoni Mwaniki akisema afisi ya DPP ilipokea faili niliyorudisha,” alisema Bw Murgor.

Mahakama ilisema kutokana na mawasilisho ya Bw Murgor ni wazi alijiuzulu na “ni jukumu la DPP kuchapisha katika gazeti rasmi la Serikali akiondoa jina la Bw Murgor katika orodha ya viongozi wa mashtaka.”

You can share this post!

Tahadhari yatolewa kuhusu kondomu mbovu

Waziri alilia viongozi wachangie kampeni ya HIV

adminleo