Habari Mseto

Sasa msiongee na fisi, KWS inakuja kuwaondoa, wakazi wa Juja waambiwa

February 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA WANDERI KAMAU

SHIRIKA la Huduma kwa Wanyamapori Kenya (KWS) limetakiwa kuharakisha mchakato wa kuwahamisha fisi ambao wamekuwa wakiwahangaisha wakazi katika eneo la Juja, Kaunti ya Kiambu.

Mnamo Ijumaa, wadau kadhaa walisema kuwa licha ya shirika hilo kuahidi kuwahamisha fisi hao mwanzoni mwa mwezi uliopita, bado kuna fisi ambao wamekuwa wakionekana wakizurura karibu na timbo za mawe katika eneo hilo.

Mwanzoni mwa Januari, shirika hilo liliwahamisha fisi 12, baada ya watu wawili kuuliwa Desemba, mwaka uliopita, hali iliyozua ukosoaji mkubwa dhidi ya shirika hilo kutoka kwa Wakenya.

Licha ya ahadi hiyo, shirika hilo linalaumiwa kwa kutowahamisha fisi wote.

Kulingana na Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Zetech, Profesa Njenga Munene, bado kuna fisi kadhaa wanaowahangaisha wanafunzi wa chuo hicho wanaoishi katika eneo la Juja.

Kwenye kikao cha wadau kadhaa kilichofanyika katika chuo hicho Ijumaa, Prof Munene alisema kuwa wanafunzi kadhaa katika taasisi hiyo wameripoti kuwaona fisi wakizurura, hasa katika eneo la Witeithie.

“Mara kwa mara, wanafunzi huwa wanatoka chuoni wakiwa wamechelewa, jambo linalowaweka kwenye hatari ya kushambuliwa na wanyama hao. Tunairai KWS kuharakisha mchakato wa kuwahamisha wanyama hao ili kuzuia visa vyovyote vya wanafunzi ama wakazi kushambuliwa,” akasema.

Alisema kuwa shirika hilo pia linafaa kuweka ua katika mbuga ya wanyama ya Ol Donyo Sabuk, kwani baadhi ya wanyama wamekuwa wakitoroka kutoka mbuga hiyo na kuwashambulia wenyeji.

“Ikiwa uhamishaji huo hautaharakishwa, basi tutalazimika kuwaua wanyama hao sisi wenyewe. Hatutangoja hadi watuletee maafa,” akasema Prof Njenga.

Hata hivyo, Naibu Kaunti Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Juja, Wilson Mwangi, aliwahakikishia wadau hao kwamba KWS inafanya kila juhudi kuwadhibiti wanyama hao.

Kwenye tahadhari kwa wenyeji hapo awali, KWS ilikuwa imerai wenyeji kuongea na fisi kama njia ya kuwafukuza.