Habari Mseto

Savula na wake zake wakana kumumunya mamilioni ya serikali

October 30th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MUNGUTI

MBUNGE wa Lugari Ayub Savula na wake zake wawili walishtakiwa Jumatatu pamoja na aliyekuwa katibu wizara ya utangazaji Sammy Itemere kwa kufanya njama ya kuibia Serikali zaidi ya Sh122.3 milioni.

Bw Savula , wake zake Bi Melody Gatwiri Ringera na Hellen Jepkor Kemboi walikanusha mashtaka ya kuibia Serikali Sh122, 335,500 wakidai watapeperusha matangazo ya wizara mbali mbali kupitia kampuni zao saba za uanahabari.

Bw Ayub , Melody na Hellen ni wakurugenzi wa The Sunday Publishers Limited, Melsav Company Limited, Johnnewton Communications , The Express Media Group, No Burns Protection Agencies Limited, Cross Continents Ventures Limited na Shieldlock Limited.

Bw Savula (kulia) na katibu mkuu wa zamani Sammy Itemere. Picha/ Richard Munguti

Mbunge huyo pamoja, wake zake na kampuni zao walikabiliwa na mashtaka matatu ya kupokea pesa Sh122,335,500 kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa Wizara ya Habari na Utangazaji kati ya Julai 1, 2015 na Agosti 31 2018 kwa kudanganya wangetoa huduma za matangazo kwa Serikali.

Katika kipindi hicho hicho wakurugenzi hao na kampuni zao walijaribu kuifuja Serikali Sh119,000,000 wakijifanya wangelichapisha matangazo ya Serikali katika majarida yanayosambazwa kote nchini.

Bw Itemere, Bw Savula, Melody, Hellen na wakuu wengine wa wizara ya utangazaji walikanusha mashtaka 10 dhidi yao na kuachiliwa kwa dhamana na Hakimu Mkuu katika mahakama ya Milimani Nairobi, Bw Francis Andayi.

Washtakiwa wote wakiwa kizimbani. Picha/ Richard Munguti

Bw Savula ndiye aliwachiliwa kwa kiwango cha juu cha pesa Sh1.5 milioni pesa tasilimu kwa vile alijibu mashtaka kwa niaba ya kampuni zake saba za uchapishaji.

Wengine wote ikiwa ni pamoja na wake zake waliachiliwa kwa dhamana ya Sh1milioni pesa taslimu.

Endapo watashindwa kupata pesa hizo washtakiwa waliagizwa wawasilishe mahakamani dhamana ya Sh2milioni.

Katika shtaka la kwanza washtakiwa wote 30 walikabiliwa na shtaka la kufanya njama za kuibia Serikali Sh 122,335,500.

Hakimu Mkuu katika mahakama ya Milimani, Nairobi, Bw Francis Andayi. Picha/ Richard Munguti

Bw Itemere, Bw Dennis Kuko Chebitweny, Dickson Onjala Nyandiga, Henry Musambanga Mungasia, Fredrick Okello Owiti,Edith Kainda Nkanata,Amos Matanga Tayari, Susan Akinyi Ouma, Gladya Hadida Bwor, Gladys Isaka Mwanyika,Agren Jescar Ateka,Rachael Wanjiru Munge na Nellie Nyachoba Kiboka walikana kufadhili kampuni za Bw Savula na kuifuja Serikali pesa hizo.

Wengine waliokana mashtaka ni Sammy Makau Mule,Tabitha Nyaboke Oriba,Martin Njoroge Njenga,Hannah Wangari Wanderi, Edmund Horrace Munene na Joseph Kamau.

Mabw Itemere, Chebitwey, Nyandika,Mungasia na Akinyi walikana kutumia mamlaka yao vibaya kwa kuidhinisha malipo hayo kwa kampuni za Bw Savula.

Bw Savula, Melody na Hellen walishtakiwa tena kwa kughushi barua waliyodai imeandikwa na kutiwa saini na Bi Judith Sherry Sirma , afisa mkuu Wizara ya Afya ikiidhinisha matangazo.

Mawakili wa washtakiwa. Picha/ Richard Munguti

Kiongozi wa mashtaka Bw James Warui Mungai hakupinga washtakiwa kuachiliwa kwa dhamana.

Kesi hiyo itatajwa Desemba 6, 2018 kwa maagizo zaidi na kutoa mwelekeo wa tarehe ya kusikizwa kwake.

Aliomba hakimu aamuru washukiwa watano ambao hawakujisalamisha kwa afisi ya mkurugenzi wa uchunguzi wa jinai(DCI) wafike huko leo saa moja asubuhi wachukuliwe alama za vidole na kushtakiwa rasmi.

Washukiwa wengine watano hawakujisalamisha na walifunga simu zao, nao wameamriwa watiwe nguvuni.

Kesi hiyo itatajwan Desemba 6, 2018 kwa maagizo zaidi na siku ya kusikizwa itengwe.

Mahakama iliamuru upande wa mashtaka uwakabidhi nakala za mashahidi washtakiwa waandae teteziu zao.