Habari Mseto

Sekta tatu ambazo huwekea wateja bei za uwongo

August 22nd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

Mamlaka ya Ushindani nchini (CAK) imetangaza kuwa asilimia kubwa ya bei katika sekta ya reja reja, viwanda na benki ni za uongo na za kupotosha.

Katika ripoti yake ya kila mwaka, mamlaka hiyo ilisema kufikia asilimia 60 ya malalamishi ya wateja inatoka katika sekta hizo tatu.

Wakati wa mwaka wa 2016/2017, mamlaka hiyo ilikabiliwa na visa 66, malalamishi kutoka kwa wateja, ambapo asilimia 50 ya visa hivyo vilitatuliwa.

Zaidi ya visa hivyo, CAK ilitangaza kuwa pia ilipokea malalamishi kuhusu ubora wa bidhaa, na habari za kupotosha kuhusu udhamini wa bidhaa, ofa na kujiunga na chaneli za kulipia za TV.

Mamlaka hiyo ilipokea malalamishi kutoka katika sekta za uchukuzi, utengezaji wa bidhaa, bima, elektroniki, maji, fedha ma kawi.

Baadhi ya malalamishi ni kuhusiana na matumizi ya salio la simu (credit) mteja anapoingia katika intaneti licha ya kuwa na salio la intaneti (bundles).

Pia, maduka ya rejareja yalipatikana kudanganya wateja katika mauzo ya majokovu ambapo yametangaza uwezo wake kwa kutumia futi badala ya lita.

Baadhi ya maduka yalipatikana kuuza bidhaa zilizoharibika kama vile meko ambayo ni vigumu kuwasha au kuzima au kupunguza moto, au matangi ya maji ambayo yanapasuka siku chache baada ya kununuliwa.