Seneta apigia debe Punguza Mizigo
Na OSCAR KAKAI
SENETA wa Kaunti ya Pokot Magharibi, Bw Samuel Poghisio ameunga mkono mapendekezo kwenye mswada wa marekebisho ya katiba wa Punguza Mizigo.
Mswada huo unaopigiwa debe na Kiongozi wa Chama cha Thirdway Alliance, Dkt Ekuru Aukot umepingwa na Gavana wa Kaunti hiyo, Prof John Lonyangapuo.
Bunge la kaunti hiyo limegawanyika kuhusu mswada huo.
Seneta huyo alisema anaunga mkono mswada huo kwa sababu utasaidia kuimarisha mgao kwenye kaunti na kuipa nguvu bunge la seneti.
Akiongea jana na wanahabari mjini Kapenguria, Bw Poghisyo alisema mswada huo utainua uchumi wa nchi, kubadilisha maisha ya Wakenya na kuhakikisha matumizi bora ya fedha.
“Wale wanapinga wana sababu za kibinafsi. Ninashukuru Aukot na kikosi chache cha wataalamu kwa kufaulu na mpango huo. Sio rahisi kukusanya sahihi kote nchini na hatuwezi kupuuza kile Aukot amefanya,” alisema.
Seneta huyo alitoa wito kwa Wakenya kuunga mkono Punguza Mizigo hadi kwenye ngazi zingine sababu kuna haja ya fedha nyingi kuenda kwenye kaunti.