• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 3:24 PM
Seneta ataka EACC ichunguze fidia ya ardhi kwa wakazi Lamu

Seneta ataka EACC ichunguze fidia ya ardhi kwa wakazi Lamu

Na KALUME KAZUNGU

SENETA wa Lamu, Anwar Loitiptip ameiandikia Tume ya Kukabili Ufisadi nchini (EACC) kuitaka ichunguze jinsi fidia za ardhi kwa wakazi walioathiriwa na miradi ya kitaifa eneo hilo, ukiwemo ule wa Bandari ya Lamu (LAPSSET) imekuwa ikitekelezwa.

Katika barua yake ambayo Taifa Leo iliona, Bw Litiptip pia anaitaka Tume ya EACC kuchunguza jinsi ardhi ambapo miradi, ikiwemo ule wa uchimbaji wa gesi eneo la Pate, mradi wa Sh21 bilioni wa nishati ya upepo eneo la Baharini, tarafa ya Mpeketoni zilivyotwaliwa.

Bw Loitiptip pia ameitaka EACC kuchunguza mpangilio unaotumiwa katika utoaji wa tenda za serikali ya kaunti ya Lamu, akidai mpangilio huo umekuwa ukikiuka hatua zinazostahili kufuatwa kabla ya tenda hizo kutolewa.

Pia anataka orodha ya majina ya waathiriwa wote ambao ardhi zao zilitwaliwa ili kupisha ujenzi wa miradi ya serikali kaunti ya Lamu kuchapishwa na kuwekwa wazi kwa umma.

Seneta huyo pia amemwomba Mwenyekiti wa EACC, Eliud Wabukala kuhakikisha tume yake imechunguza kwa makini ripoti ya ukaguzi wa kifedha katika kaunti ya Lamu kati ya mwaka wa kifedha wa 2013 hadi 2018, akidai kulikuwepo na ubadhirifu katika matumizi ya fedha za kaunti katika kipindi hicho.

Itakumbukwa kwamba mnamo Februari, 2015, serikali ya kitaifa ilitoa Sh 1.3 bilioni na kukabidhi Tume ya Ardhi nchini (NLC) ili kutoa fidia kwa zaidi ya wakazi 100 walioathiriwa na mradi wa LAPSSET eneo la Kililana na Mashunduani.

Bw Loitiptip anadai kukithiri kwa makosa mengi wakati wa utoaji wa fedha hizo huku waathiriwa halisi wakikosa kufidiwa ardhi zao.

“Naisihi EACC kuchukulia masuala haya kwa uzito. Wachunguze kwa haraka masuala mengi ya Lamu yanayohitaji uwazi na uwajibikaji.

“Baadhi ya yale yanayofaa kuchunguzwa kwa haraka ni fidia ya ardhi za miradi ya serikali, ikiwemo LAPSSET, mradi wa nishati ya upepo, mradi wa uchimbaji wa madini ya gesi na kadhalika. Pia EACC ichunguze ripoti ya uhasibu wa fedha wa kati ya mwaka wa kifedha wa 2013 hadi 2018. Pia wahakikishe wamechunguza na majina ya waathiriwa wote wa miradi ya kitaifa yachapishwe,” akasema Bw Loitiptip

You can share this post!

Waumini wamkataa askofu mpya

Polo na mkewe wapigishwa raundi baada ya kunaswa na mboga...

adminleo