Habari Mseto

Seneti kumwita Naibu Gavana aliyezama Amerika

October 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

MASENETA wameamua kumwita Naibu Gavana wa Pokot Magharibi, Nicholas Atudonyang’ kufika mbele yao kumshinikiza ajiuzulu kwa kutofika kazini tangu aingie ofisini mwaka 2017.

Hii ni baada ya Gavana wa kaunti hiyo Profesa John Lonyangapuo kuwaambia wanachama wa Kamati ya Seneti kuhusu Ugatuzi kwamba hana mamlaka ya kikatiba kumfuta kazi naibu wake wala kumshinikiza ajiondoe.

“Ni kweli kwamba naibu wangu hajakuwa kazini kwa muda mrefu. Alikuwa nchini Desemba 2018 lakini hakurejea Aprili 2019 alivyoahidi,” akasema Gavana Lonyangapuo alipofika mbele ya kamati hiyo Jumanne katika majengo ya bunge.

Akaongeza: “Mwaweza kwenda Texas, Amerika kumshinikiza ajiuzulu kwani Katiba haijanipa mamlaka ya kumwondoa ofisini na sina uwezo wa kumlazimisha ajiuzulu. Vilevile mwaweza kumwita hapa na kumlazimisha ajiondoe.”

Ataka kubuniwa kwa sheria

Prof Lonyangapua hata hivyo aliitaka kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Laikipia, John Kinyua kubuni sheria itakayowapa magavana mamlaka ya kuwafuta kazi manaibu wao.

“Wazo hilo ni nzuri lakini kabla ya hapo tunapanga kumwita naibu wako afike mbele yetu kuelezea ni kwa nini amekuwa akiishi Amerika ilhali anapaswa kuwa kazini,” akasema Seneta Kinyua, japo hakutaja ni lini Dkt Atudonyang’ atahitajika kufika mbele ya kamati yake.

Prof Lonyangapuo alisema kaunti imesimamisha mshahara wa naibu wake na kumpokonya wadhifa wa waziri wa afya katika kaunti hiyo.

“Hata hivyo, Dkt Atudonyang’ amekuwa akiisaidia kaunti yetu kwa njia nyingi licha ya kwamba hajakuwa akiripoti ofisini inavyohitaji. Kwa mfano, mwaka jana alitusaidia kupata msaada wa vifaa vya matibabu vya thamani ya Sh150 milioni kutoka shirika moja la Amerika,” akasema.

Gavana huyo alikuwa amefika mbele ya kamati hiyo kujibu malalamishi yaliyowasilishwa kwa seneti na Diwani Denis Ruto kuhusu naibu gavana huyo kutokuwa kazini.