Habari Mseto

Seneti yambandua Waititu

January 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na PETER MBURU

MASENETA Jumatano walipiga kura ya kumbandua Bw Ferdinand Waititu kama Gavana wa Kaunti ya Kiambu ambapo kwa idadi ya wingi wa kura, alikutwa na hatia ya makosa yote matatu yaliyowasilishwa na madiwani wake.

Kulikuwa na jumla ya maseneta 38 katika safu ya seneti Jumatano ambapo 28 wengi kutoka upinzani waliridhia gavana abanduliwe ofisini.

Shtaka la kwanza la kukiuka Katiba, maseneta 27 waliunga abanduliwe huku 12 wakipiga kura ya kumuondolea lawama.

Nalo la pili lilihusu ukiukaji wa sheria za nchi ambapo 28 walipiga kura abanduliwe huku 11 wakipinga.

Mtindo huo wa pili wa upigaji kura ulijirudia katika shtaka la tatu la utovu wa maadili na tabia isiyopendeza,

Kwenye kikao cha Jumatano kilichoendelea hadi usiku, Waititu alijitetea vikali na kusema maseneta hawakuwa na mamlaka ya kuamua kuhusu hoja yenyewe.

Baada ya kusikiza mashtaka yaliyowasilishwa na Bunge la Kaunti ya Kiambu na utetezi wa Gavana Waititu kwa siku mbili, Seneti ilifikia uamuzi wa kumwondoa ofisini kwa njia ya kumbandua.

Uamuzi huo ulitoa fursa kwa maseneta kupiga kura kuamua mustakabali wa Bw Waititu, mjadala ulioendelea hadi usiku (muda wa kuchapisha gazeti ulipofika).

Hata hivyo, hata kabla ya wakati wa kupiga kura kufika, maseneta walikuwa wakijibizana kuhusu uamuzi huo wakitoa hoja zao, huku tofauti za kisiasa zikionekana, kwani waliokuwa wakimtetea ni wafuasi wa Naibu Rais William Ruto pekee.

Waliokuwa wakiunga mkono kubanduliwa kwa Waititu, walimkosoa kuwa alichukulia suala hilo kwa wepesi na kuwa hakuwasilisha ushahidi wa kukabili madai yaliyowasilishwa na bunge la kaunti kwa muda uliofaa.

“Hatuko hapa kumsaidia, ila kufuata sheria,” Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Jr akasema.

Baadhi ya waliokuwa wakimtetea Bw Waititu ni kiongozi wa wengi Seneti Kipchumba Murkomen, seneta wa Nakuru Susan Kihika na wa Kericho Aaron Cheruiyot ambao waliungama na madai ya mawakili wake kuwa Bunge la Kaunti ya Kiambu halikufuata utaratibu lilipomtimua.

“Sharti tukague ushahidi ikiwa Bunge la Kaunti lilifuata sheria na kutoa uamuzi unaofaa,” akasema.

Waititu na mawakili wake wakimtetea, suala la kukiukwa kwa utaratibu wa kisheria wakati Bunge la Kaunti ya Kiambu lilimbandua lilitawala.

Walisema bunge hilo lilikongamana kufanya uamuzi huo baada ya muda unaoruhusiwa kisheria, hatua iliyofanya uamuzi wa siku hiyo kuwa haramu, mbali na kusema kuwa madiwani waliokuwapo bungeni siku hiyo hawakutimiza idadi inayohitajika kupitisha hoja ya kumbandua gavana, na kuwa mawakili wa Bw Waititu waliokuwa wamefika kumtetea walinyimwa fursa ya kuzungumza.

“Madiwani 35 hawakuwapo bungeni siku hiyo na hivyo idadi ya waliokuwapo haikufika thuluthi mbili inavyohitajika kisheria. Kwa kuangazia jinsi hali ilivyokuwa, Bunge la Kaunti ya Kiambu halikumbandua Gavana Waititu (kisheria). Hoja na uamuzi wa kumbandua vilikiuka utaratibu na hivyo vinafaa kutupiliwa mbali,” akasema wakili Ng’ang’a Mbugua.

Vilevile, mawakili wa Bw Waititu walikosoa Seneti kuwa ilichelewa kuandaa kikao cha kusikiza hoja hiyo zaidi ya muda unaoruhusiwa kisheria, na hivyo haikuwa na mamlaka ya kuisikiza na kuiamua tena.

“Seneti ilichelewa kuandaa kikao hiki kwa siku 28 na hivyo, kisheria, haina mamlaka ya kuamua suala hili. Uamuzi wa spika kuandaa kikao hiki sasa ulikiuka kipengee cha 33 cha sheria ya serikali za kaunti,” akasema.

Bw Waititu naye mbeleni alidokeza kuwa huenda alipanga kufika kortini endapo angebanduliwa, akisema “Naomba bunge hili kutoa uamuzi ambao hauwezi kupingwa kortini.”

Saa za asubuhi, seneta maalum Isaac Mwaura alikuwa ametuma ujumbe kwenye akaunti yake ya Twitter, akiashiria kuwa Bw Waititu angeadhibiwa, suala ambalo lilizua ubishi kutoka kwa Bw Waititu baadaye.

“Tumekataa ombi la Waititu kuleta ushahidi baada ya muda kuisha. Wakazi wa Kiambu wanahitaji haki. Waititu atakabiliana na sheria kikamilifu. Hakuna mwizi anafaa kuepuka kuadhibiwa,” seneta Mwaura akaandika.

Katika mengi ya maneno yake, Bw Waititu alikuwa akiwalaumu madiwani kuwa wanaompiga na kuwatahadharisha maseneta kuhusu uamuzi ambao wangetoa.

“Mtakavyoniamulia leo itawaadhiri baadaye mtakapokuwa magavana,” akasema.

Bw Waititu alibanduliwa mnamo Desemba 19 mwaka jana, kwa madai ya kutumia ofisi vibaya, kuajiri wafanyakazi wa vibarua bila kufuata sheria na kupeana tenda za mamilioni kwa watu wa familia yake.

Tangu serikali za ugatuzi zilipoanza kazi, Seneti imeidhinisha hoja ya kumbandua Gavana Martin Wambora pekee, japo Mahakama ilimrejesha baadaye ilipoamua kuwa hakukuwa na ushahidi wa kutosha kumbandua.

Magavana wengine ambao wamefika mbele ya seneti kwa hoja za kubanduliwa ni Paul Chepkwony (Kericho), Mwangi Wa Iria (Murang’a), Marehemu Nderitu Gachagua (Nyeri) na Granton Samboja (Taita Taveta)