Serikali kurejesha treni jijini kupunguza msongamano
Na BERNARDINE MUTANU
SERIKALI imetangaza kuanzisha mpango wa kuanzisha tena uchukuzi kwa njia ya treni Jijini Nairobi.
Waziri wa Uchukuzi James Macharia Jumanne alisema serikali imechagua kuanzisha magari mengi ya moshi badala ya mabasi kwa lengo la kupunguza msongamano jijini.
Bw Macharia alisema makatibu wakuu kutoka Wizara ya Uchukuzi na Muundo Msingi tayari wameenda Uhispania kwa lengo la kumalizia ununuzi wa magari hayo.
“Kwa sasa tunalenga njia mbili, moja ni ile ya Syokimau hadi katikati mwa jiji na nyingine ni ile ya Ruiru hadi katikati mwa jiji,” alisema.
Macharia alisema njia hizo mbili zitatoa uchukuzi mbadala baada ya kusimamisha mpango wa kuanzisha uchukuzi kwa njia ya mfumo maalum wa Rapid Transit System –RTS.
Hata hivyo, alisema magari hayo sio eti yanachukua mahali pa mabasi hayo (Bus Rapid Transit-BRT).