Serikali kusafirisha waombolezaji hadi Kabarak
NA ERICK MATARA
SERIKALI imetangaza kwamba mipango yote ya mazishi ya Rais wa pili wa Kenya Daniel Arap Moi yanayotarajiwa kufanyika kesho nyumbani kwake Kabarak, Kaunti ya Nakuru imekamilika.
Kamishna wa eneo la Rift Valley George Natembeya alisema jana kuwa serikali itatoa magari ya kuwasafirisha raia kutoka mji wa Nakuru hadi Kabarak kwa ajili ya mazishi hayo.
“Mabasi ya shule na magari mengine yakiwemo yatakayotolewa na Kaunti ya Nakuru yatawasafirisha raia hadi eneo la mazishi Kabarak. Magari hayo yataabiriwa katika maeneo teule ambayo yatatajwa Jumanne. Nawaomba wenyeji wajitokeze kwa wingi kusheherekea maisha ya Mzee Moi,” akasema Bw Natembeya.
Kwa mujibu wa Bw Natembeya, waombolezaji watakaofika Kabarak watapewa maji ya kunywa, vitafunio na eneo la kuegesha magari yao.
Ikizingatiwa kwamba halaiki ya watu inatarajiwa kuhudhuria mazishi hayo, msongamano mkubwa wa magari unatarajiwa kwenye barabara kuu ya Nairobi – Eldoret leo na kesho.
Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai tayari ametangaza kuwa malori na matrela hayataruhusiwa kutumia barabara hiyo leo na kesho.
Mwili wa Mzee Moi utasafirishwa kwa ndege hadi nyumbani kwake Kabarak kesho asubuhi huku maombi ya makanisa mbalimbali yakiandaliwa kwa heshima yake leo uwanjani Nyayo.
Wakazi wa maeneobunge ya Baringo ya Kati na Baringo Kaskazini, ambayo yaliwakilishwa bungeni na Mzee Moi kwa muda wa miaka 39, watafuatilia mazishi yake kwenye runinga kubwa itakayowekwa katika Shule ya upili ya Sacho.
Runinga hizo pia zitawekwa katika uwanja wa Afraha na Kabarak kwa raia kufuatilia mazishi hayo.