Habari Mseto

Serikali ya kaunti ya Bomet yamulikwa kuhusu ubadhirifu wa Sh9m kwa fanicha

December 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MARY WANGARI

GAVANA wa Bomet Hillary Barchok huenda akajipata mashakani miezi michache tu baada ya kuchukua usukani kufuatia ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kufichua kiongozi huyo alitumia Sh9.9 milioni kulipia samani ofisini mwake.

Hata hivyo, alijieleza akisema hafai kulaumiwa na kwamba uagizaji ulifanywa akiwa bado kuingia mamlakani.

Aidha, aliyekuwa gavana wa kwanza wa Bomet, Isaac Ruto, inadaiwa aliagiza dawati kwa Sh750,000.

Bw Barchok aliyechukua hatamu mnamo Agosti 2019 kufuatia kifo cha aliyekuwa Gavana Joyce Laboso, alifika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Fedha za Umma na Uwekezaji mnamo Jumanne.

Kamati hiyo iliyoongozwa na Seneta wa Kaunti ya Homa Bay Moses Kajwang, ilimtaka gavana huyo kujibu maswali kuhusu ripoti iliyotolewa na aliyekuwa Mkaguzi Mkuu Edward Ouko katika bajeti ya kati ya 2017 na 2018 iliyoibua ubadhirifu mkuu wa fedha za umma.

Kulingana na kamati hiyo ni kwamba kaunti ilitumia Sh50 milioni kwa ofisi ya gavana pamoja na Sh24 milioni kwa bustani; kiasi ambacho ni sawa na ada za uegeshaji magari kwa mwaka mmoja.

Aidha, iliibuka kuwa iliwagharimu wapigakura Bomet kiasi cha Sh755,000 kununua kiti cha gavana, Sh398,000 kununua kiti cha naibu wake pamoja na Sh0.5 milioni kununua meza.

Dawati la gavana liligharimu Sh0.7 milioni, rafu ya vitabu Sh0.4 milioni, viti vya mkutano Sh1.1 milioni, bilauri za maua Sh57,000, meza za mikutano Sh800,000 pamoja na bidhaa za usafirishaji Sh23 milioni.

“Bahati ilioje kuwa msaidizi wa gavana? Gavana wa Bomet ana kochi la kifahari la ngozi linaloweza kukaliwa na watu sita lililotengenezwa kwa mbao za mahogany na kutiwa nakshi kikamilifu lenye thamani ya Sh755,000,” alifichua Bw Kajwang.

Akizungumza katika kikao hicho cha kamati, Seneta wa Narok Ledama Ole Kina alihoji kwamba ingekuwa vigumu kwa Bw Barchok kuangamiza umaskini eneo hilo endapo angeendelea kufuja kiholela fedha za umma.

“Ikiwa unatumia mapato yaliyotengewa watu 1,430 kununua samani, hakuna jinsi utaweza kuziba pengo kati ya maskini na matajiri Bometi,” alihoji Bw Ole Kina.

Barchok akajitetea.

“Uagizaji wa bidhaa hizi ulifanywa mnamo kipindi ambacho sikuwa mamlakani. Wafanyabiashara walilipwa baada ya kuwasilisha stakabadhi halali,” akasema Barchok.

Maseneta mbalimbali waliokuwepo katika kikao hicho cha kamati akiwemo Seneta wa Kiambu Kimani Wamatangi walielezea wasiwasi wao kuhusu ubadhirifu uliokithiri wa fedha za umma hata katika maeneo mengine wakiwataka wakaguzi kumakinika ili kulinda fedha za umma.

“Bilauri ya maua kwa Sh60,000 ili tu kushikilia maua katika kaunti ya mashinani? Na wanapoketi kwenye dawati hizo, mama maskini anapowaomba ufadhili wa masomo, unajua wao humpa kiasi kipi? Sh2000!” alihoji Seneta Wamatangi.

Gavana Barchok kwa upande wake alieleza kamati hiyo kwamba mchakato wa ununuzi ulikuwa ukichunguzwa.