Habari Mseto

Serikali yaanza kupata vizingiti kutekeleza ushuru kwa wakulima

February 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA WANDERI KAMAU

SERIKALI imeanza kupata vizingiti katika kutekeleza ushuru kwa wakulima, baadhi yao wakisema inaenda kinyume na ahadi ilizotoa kwao kuhakikisha inainua maisha yao.

Wakulima hao wanalalamikia hatua mpya, ambapo wataanza kukatwa ushuru kwa mapato yao kupitia mfumo mpya wa kielektroniki wa ushuru (e-TIMS).

Katika eneo la Mlima Kenya, ambalo ni miongoni mwa ngome za utawala wa Kenya Kwanza, wakulima wengi waliozungumza na Taifa Leo walisema kuwa kwa kutekeleza mfumo huo mpya, serikali inaenda kinyume na ahadi yake ya “kuwainua watu wa kiwango cha chini”.

Baadhi yao wameapa kutowasilisha mapato yao, huku wengine wakimrai Rais William Ruto kutathmini athari za baadhi ya sera za ushuru zinazotekelezwa na serikali yake.

“Kwa kweli, hizi ni sera zitakazowafinya sana wakulima. Ikumbukwe kuwa, wengi wetu huwa tunategemea kilimo kwa shughuli muhimu kama kulipa karo na mahitaji ya kila siku. Sijui tutaelekea wapi sera hii mpya ikianza kutekelezwa,” asema Bi Milcah Muthoni, ambaye ni mkulima katika Kaunti ya Kiambu.

Katika eneo la Kandara, Kaunti ya Murang’a, maafisa wa Halmshauri ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) walikuwa na kibarua kigumu kuwafahamisha wakulima kuhusu taratibu ambazo watakuwa wakifuata katika kuwasilisha mapato yao kwa serikali kupitia e-TIMS.

Baadhi ya wakulima walisema kuwa mapato yao ni ya kiwango cha chini, hivyo serikali haifai kuwajumuisha miongoni mwa Wakenya wanaolipa ushuru.

“Sisi ni watu ambao mapato yetu hayatabiriki. Leo umepata, kesho umekosa. Ni vipi utaanza kumtoza ushuru mtu kama huyo? Ombi letu ni sera hiyo kutathminiwa tena,” akasema Bw James Gichuki, ambaye ni mkazi wa Kaunti ya Nyandarua.