Serikali yahimizwa kutolegeza kamba vita dhidi ya ufisadi
Na LAWRENCE ONGARO
SERIKALI imeanza kuonyesha juhudi za kupambana na ufisadi, lakini wafanyabiashara na viongozi wa Thika wanaitaka izidi kutia bidii.
Wakiongozwa na mwenyekiti wa wafanyabiashara mjini Thika, Bw Alfred Wanyoike, walisema uamuzi wa mahakama kuhusu maswala ya ufisadi kwa kumhukumu mbunge wa Sirisia kifungo cha jela ni mojawapo ya ishara ya kwamba mahakama imeanza kuwa na makali yake ili kukabiliana na janga la ufisadi.
Mbunge huyo wa Sirisia alikabiliwa na kesi iliyohusu ulaghai wa wizi wa mahindi kutoka kwa Bodi ya Nafaka na Mazao Nchini (NCPB) ambapo zaidi ya Sh314 milioni zilifujwa.
“Tumeanza kuona mahakama ikionyesha makali yake. Tunataka kuona mahakimu na majaji wakitekeleza wajibu wao bila kuingiliwa na yeyote,” alisema Bw Wanyoike.
Alisema ufisadi umeponza juhudi za serikali kufanya maendeleo ipasavyo na ndiyo maana haufai kupewa nafasi kushamiri.
Aliyasema hayo mnamo Alhamisi mjini Thika alipokuwa akitathmini jinsi wafanyabiashara wanavyojiandaa kufungua biashara zao wakati wowote.
Alisema ufisadi umesababisha biashara nyingi kufungwa.
Aliwataka viongozi wasiingilie serikali ikipambana na ufisadi bali waache vitengo husika viendeshe uchunguzi wao bila kuingiliwa.
Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina alikuwa amewasilisha mswada bungeni kuwa mafisadi wapewe adhabu kali huku wabunge wengine wakikubaliana naye.
Alisema iwapo nchi haitakabiliana na ufisadi vilivyo bila shaka “hatutaweza kufanya maendeleo muhimu hapa nchini.”
“Iwapo serikali itawatupa jela miaka kadha viongozi wawili hivi, lakini mashuhuri wanaojihusisha na ufisadi, bila shaka ufisadi katika ngazi ya juu utakwisha,” Bw Wainaina alisema.
Bi Shaleen Wanjiru, ambaye ni mfanyabiashara mjini Thika alisema serikali haifai kuwasaza viongozi wachache kutokana na ufisadi lakini iwakabili bila huruma.
“Ufisadi ndio umesababisha vijana wengi na hata walemavu kukosa ajira. Kwa hivyo, mafisadi wakabiliwe vilivyo,” alisema Bi Wanjiru.