• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 9:11 AM
Serikali yaonya kuhusu wajenzi wasiosajiliwa

Serikali yaonya kuhusu wajenzi wasiosajiliwa

Na SHABAN MAKOKHA

SERIKALI imeonya wawekezaji katika sekta ya ujenzi dhidi ya kutumia wanakandarasi bandia.Waziri wa Leba Simon Chelugui alisema, wahandisi ambao hawajasajiliwa ndio hutengeneza majengo duni yanayohatarisha maisha ya wananchi.

Alisema serikali imejitolea kusafisha uozo uliopo katika sekta ya ujenzi ili kuhakikisha wajenzi halali pekee ndio wanapewa kandarasi. Akizungumza katika Taasisi ya Mafunzo ya Kiufundi ya Chamasiri, Teso Kaskazini, Kaunti ya Busia jana, waziri alisema wawekezaji wanaotumia wajenzi bandia pia hupata hasara tele.

Alisema idadi kubwa ya wajenzi kama hao huwa ni wa humu nchini, ambao pia husababisha miradi ya ujenzi kukwama hasa katika sekta ya umma.

“Kumekuwa na majengo duni ambayo huporomoka kiholela kutokana na ongezeko la ufisadi,” akasema.Alisema wengi wa wajenzi hao huwa hawana ujuzi wa kiufundi wala uwezo wa kifedha kufanikisha miradi wanayopewa.

Kulingana na Bw Chelugui, Sheria inayosimamia Mamlaka ya Kitaifa ya Ujenzi inafaa kutumiwa kikamilifu na wadau wa sekta hiyo ili kuondoa wajenzi bandia.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, wajenzi wasiofuata kanuni za kitaaluma huwa wanafaa kuondolewa kwenye sajili ili wasipate kandarasi kwingine baada ya kushindwa kutekeleza wajibu wao.

Wakati huo huo, Bw Chelugui alisema serikali imebuni mtandao wa kutoa mawaidha kwa vijana kuhusu masuala ya leba.Alisema mtandao huo unatoa mawaidha kuhusu kazi humu nchini na hata nje ya nchi, na akashauri vijana wautumie kuepuka kudhulumiwa na waajiri.

You can share this post!

LSK yataka majaji wapya kabla 2021

Wakenya Amerika wagawanyika wamchague Trump au Joe Biden