Habari Mseto

Serikali yaonya wachochezi kwenye mzozo wa malisho

June 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LUCY MKANYIKA

SERIKALI imeonya wanasiasa wa kaunti ya Taita Taveta dhidi ya kuchochea mzozo unaoendelea kati ya wenyeji na wafugaji haramu.

Vikosi vya usalama katika eneo hilo vinachunguza baadhi ya wanasiasa ambao wanadaiwa kuhusika katika visa vya utovu wa usalama vinavyoendelea katika eneo hilo.

Akiongea na wanahabari, kamishna wa kaunti hiyo Bi Rhoda Onyancha alisema kuwa hawatachelewa kuwachukulia hatua viongozi watakaopatikana kuhusika katika visa hivyo.

Bi Onyancha alisema kuwa serikali iko macho kuona kuwa hali ya kawaida inarejea katika eneo la Sagalla ambalo linashuhudia mzozo baina ya wachungaji ngamia na wakulima.

Haya yanajiri baada ya wachungaji wawili kuvamiwa na kujeruhiwa na watu wasiojulikana bomani kwao.

Wawili hao walikatwakatwa kwa panga na kisha kutibiwa katika hospitali ya Moi mjini Voi.

Inadaiwa kuwa baadhi ya wenyeji wameapa kuwafurusha wachungaji ngamia waliovamia kaunti hiyo kulisha mifugo wao.

Bi Onyancha alisema kuwa mtu mmoja amekamatwa kutokana na tukio hilo.

“Mshukiwa atafikishwa mahakamani Jumatatu. Tunaendelea na uchunguzi na hatutaogopa kukamata yeyote hata kama ni mwanasiasa,”akaonya.

Wakati wa tukio hilo, wavamizi vilevile walichoma mali ya wachungaji hao ikiwemo magodoro na vyombo vya nyumbani.

Haya yanafuatiwa na kifo cha mkulima mmoja aliyedaiwa kuuliwa na wachungaji ngamia shambani kwake katika eneo la Kirumbi, wadi ya Sagalla.

Wafugaji hao walikadiria hasara baada ya ngamia wao vilevile kupatikana wameuliwa kwa kile kilichoonekana kama kisa cha kulipiza kisasa na wenyeji wa eneo hilo.

Hali ya taharuki imetanda katika eneo hilo huku baadhi ya wenyeji wakiripoti kuwa wanahofia maisha yao.

Mwakilishi wa wadi hiyo Bw Godwin Kilele amekuwa akidai kuwa maisha yake yako hatarini.

Hata hivyo kiongozi huyo hajaandikisha taarifa yeyote kwa polisi. Bi Onyancha alisema kuwa polisi wameimarisha doria katika eneo hilo ili kutuliza hali.

“Hakuna mtu yeyote ambaye ameripoti kuhusu kutishiwa maisha. Tunaomba wenyeji na wafugaji wadumishe amani,” akasema.

Wiki jana serikali iliahidi kuwa itawafurusha wafugaji haramu wanaoleta mzozo katika eneo hilo.

Serikali iliwataka wamiliki wa renchi katika kaunti hiyo kutoa orodha ya wafugaji wanaolisha mifugo wao katika renchi hizo.

Walitakiwa kutoa nakala za makubaliano baina yao na wafugaji ili kujua wafugaji halali.

Mwenyekiti wa maeneo ya uhifadhi katika kaunti hiyo Bw Mcharo Bong’osa alisema kuwa watatimiza amri hiyo mara moja.

Bw Bong’osa hata hivyo alilaumu serikali kwa kuchukua muda kutatua mzozo huo ambao umesababisha wenyeji kuuliwa na mimea yao kuharibiwa.

“Sisi kama wamiliki wa renchi za eneo hili hatukubali mifugo haramu kulisha bila makubaliano,” akasema.

Serikali vilevile imeanzisha mikutano ya amani baina ya wachungaji, wenye ngamia na wenyeji ili kuzuia mzozo zaidi kuendelea.

Naibu kamishna wa Voi Bw Joseph Mtile alifanya majadiliano na wafugaji hao ili kupanga mikutano katika vijiji mbalimbali ambapo wafugaji hao hulisha ngamia wao.

Viongozi wa kaunti hiyo wakiongozwa na gavana Granton Samboja walitoa onyo kali kwa wafugaji wanaolisha mifugo wao mashambani kuwa watachukuliwa hatua za kisheria.