Habari Mseto

Serikali yarudisha vuta pumzi baada ya ajali kuongezeka

October 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na BENSON MATHEKA

MADEREVA wanaoendesha magari wakiwa walevi watajipata pabaya baada ya serikali kurejesha kifaa cha kupima kiwango cha pombe mwilini almaarufu vuta pumzi.

Kifaa hicho kiliacha kutumiwa 2017 baada ya mahakama kuamua kwamba kilikuwa kikitumiwa kinyume cha sheria.

Mamlaka ya kitaifa kuhusu uchukuzi na usalama (NTSA) na polisi zimeamua kurejesha kifaa hicho, baada ya kubainika kuwa ajali za hivi punde zinasababishwa na madereva kuendesha magari wakiwa walevi.

Kulingana na NTSA Watu 60 walikufa kwenye ajali za barabarani kwa sababu ya ulevi kati ya Oktoba 2 na 4.

Kwenye taarifa, NTSA na polisi zilisema kwamba kifaa hicho kitatumiwa katika barabara za miji mikubwa ili kukabiliana na ongezeko la ajali.

Hii inafuatia ongezeko la ajali baada ya Rais Uhuru Kenyatta kulegeza kupunguza saa za kafyu kutoka saa tatu usiku hadi saa tano usiku.

“Rekodi zinaonyesha kwamba kuanzia Oktoba 2 hadi Oktoba 4 2020, watu 60 walikufa kwenye ajali na nyingi zilihusishwa na madereva kuendesha magari wakiwa walevi,” ilisema taarifa ya serikali.

Takwimu za NTSA zinaonyesha kuwa watu 2,689 walikufa kwenye ajali za barabarani kati ya Januari na Septemba 2020 ikilinganishwa na 2,655 waliokufa katika kipindi hicho mwaka jana.

Kulingana na takwimu hizo, idadi ya wanabodaboda na abiria wao waliokufa kwenye ajali iliongezeka kwa asilimia 44.94 na 19.44 mtawalia.

Kufuatia ongezeko hili, polisi wameagizwa kuzidisha operesheni kuhakikisha sheria za usalama barabarani zinazingatiwa kikamilifu.

Mwaka 2019 wakuu wa polisi kaunti ya Nairobi waliagizwa warudishe vifaa hivyo makao makuu ya trafiki.

Hii ilifuatia madai kwamba maafisa wa polisi walikuwa wakiweka vizuizi visivyofaa barabarani kupokea hongo na kuruhusu madereva walevi kuendesha magari.