Serikali yasema Huduma Namba itaboresha maisha ya Wakenya
Na SAMMY WAWERU
RAIS Uhuru Kenyatta amehimiza bunge la kitaifa kupitisha mswada wa kulinda data za Huduma Namba.
Kiongozi huyo wa nchi amesema hayo Jumanne, Oktoba 20, 2020, katika maadhimisho ya Sikukuu ya Mashujaa Dei 2020, baada ya kukabidhiwa rasmi kadi yake ya Huduma Namba.
Mbali na Rais Kenyatta, mkewe kiongozi wa nchi Margaret Kenyatta na Wakenya wengine 10 wamekuwa wa kwanza kukabidhiwa kadi ya Huduma Namba.
“Tulizindua Huduma Namba ili kurahisisha utoaji wa huduma za umma kwa wananchi. Wakenya wataweza kupokea huduma huku wakiendelea na baishara na kazi zao,” amesema Rais Kenyatta.
Aidha, Rais Kenyatta amehimiza bunge la kitaifa kupitisha mswada wa kulinda data ya kila Mkenya kwenye Huduma Namba, baada ya kesi kuhusu usalama wa data na maelezo ya mtu binafsi kuwasilishwa kortini.
Mahakama Kuu mapema mwaka 2020 iliagiza bunge la kitaifa kupitisha mikakati na sheria zitakazolinda data na maelezo ya mtu binafsi kwenye Huduma Namba.
“Huduma Namba sasa ni tayari, mmeshuhudia nimepata kadi yangu. Ninatumai bunge litapitisha mswada uliowasilishwa kuhusu mikakati ya mpango huu wa kuimarisha utoaji huduma,” amesema Rais.
Usajili wa Huduma Namba ulizunduliwa mwaka wa 2018, ambapo Wakenya walihimizwa kujisajili.