Serikali yashirikisha viongozi wa dini kukabiliana na ugaidi
Na CAROLINE WAFULA
IDARA ya Kitaifa ya Kupambana na Ugaidi (NCTC) imeanza kushauriana na makundi ya kidini kote nchini ili kuhamasisha umma kuhusu hitaji la kuwajibika katika kukabiliana na ugaidi.
Shirika hilo lilikamilisha mkutano na makundi ya kidini katika maeneo ya Nyanza na Magharibi mjini Kisumu wiki hii ambapo liliomba viongozi wa kidini wawe kwenye mstari wa mbele katika juhudi za kukabiliana na ugaidi katika jamii.
Naibu Mkurugenzi wa NCTC, Bw Joseph Opondo alisema kwamba makundi ya kidini yana umuhimu mkubwa katika juhudi hizo na hivyo basi yanahitajika kuwa na umoja.
Alisema dini haifai kutumiwa kugawanya Wakenya katika vita dhidi ya ugaidi.
“Watu hawafai kugawanywa kwa misingi ya dini. Kilicho muhimu ni kwamba adui hapaswi kupewa nafasi ya kututumia kwa kutugawanya kwa misingi ya kidini,” akasema katika Hoteli ya Severeign ambako NCTC iliandaa mkutano wa siku mbili na makundi ya kidini.
Huu ulikuwa ni mkutano wa kwanza wa aina hiyo katika eneo hilo, baada ya mkutano mwingine uliofanywa kati ya shirika hilo na asasi za kiusalama za maeneo ya Nyanza na Magharibi mwa nchi.
Mashauriano hayo kuhusu ugaidi yanaendelezwa kwa ufadhili wa Muungano wa Ulaya (EU).
Askofu Mkuu Philip Anyolo wa Kanisa Katoliki, Dayosisi ya Kisumu alisema kwamba jukumu la kupambana na ugaidi katika eneo hilo limo mikononi mwa viongozi wa kidini kwa ushirikiano na wananchi.
“Lazima tujitwike jukumu kubwa katika suala hili. Tunafanya hivi kwa sababu ni hitaji kutoka kwa Mungu aliye mkuu kutuliko sisi sote,” akasema.
Maelewano
Aliongeza kwamba itakuwa muhimu kuwepo mashauriano kama hayo na kutafuta maelewano ya pamoja ni muhimu kwa dini zote.
“Huenda mwingine akauliza iwapo kuna ugaidi katika eneo letu. Jibu ni ndio. Lakini si katika eneo hili pekee. Maeneo mengi ya nchi yetu hukumbwa na hali hii kwa sababu tofauti iwe ni kisiasa, kidini, kiuchumi au kwa sababu ya uhaba wa mali asili,” akasema.
Kulingana naye, wanaojihusisha katika mambo haya hutumia mbinu za kupotosha katika imani za kidini, kuchochea uadui katika jamii tofauti na kisiasa ili kufanikisha mipango yao na kusajili wafuasi katika makundi yao.