Serikali yashtakiwa tena kuhusu Huduma Namba
Na JOSEPH WANGUI
MPANGO wa serikali wa kuhakikisha kuwa wananchi wote wanapewa nambari maalum za kuwatambulisha almaarufu Huduma Namba, bado unakabiliwa na changomoto baada ya makundi mawili ya kutetea haki za umma kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu kuidhinisha utekelezaji wa mpango huo.
Shirika la The Nubian Rights Forum na Tume ya Kutetea Haki za Kibinadamu Kenya zimewasilisha kesi katika Mahakama ya Rufaa kupinga uamuzi uliotolewa Januari 31, 2002 kuwa serikali iko huru kutekeleza mfumo huo wa usajili wa watu kidijitali, japo kwa masharti fulani.
Masharti hayo ni kwamba serikali iandae kanuni madhubuti itakayosimamia utekelezaji wa mfumo huo wa usajili (NIIMS).
Mahakama ya Rufaa imeyafaa makundi hayo baada ya Jaji Wanjiri Karanja kusema kuwa kesi yao iliyodaiwa kuwasilishwa kuchelewa sasa itachukuliwa kama iliyowasilisha kwa wakati ufaao.
“Rufaa hiyo ina mashiko na imeibua masuala muhimu ya kikatiba ambayo sharti yashughulikiwe na mahakama hii,” akasema Jaji huyo wa Mahakama ya Rufaa alipokuwa akiongeza muda ambao walalamishi wanahitaji kuwasilisha kesi yao.
Kesi hiyo ya rufaa inatokana na uamuzi uliotolewa na majaji watatu wa Mahakama Kuu kwamba shughuli ya ukusanyaji wa chembejeni (DNA) na ramani ya wanakoishi ilikiuka katiba.
Vilevile, makundi hayo yanasema sehemu fulani za Sheria ya Usajili wa Watu inayohitaji ramani ya wanakoishi na DNA inakiuka kipengele cha 31 cha Katiba na hivyo usajili wa Huduma Namba ni kinyume cha Katiba.
Majaji Weldon Korir, Pauline Nyamweya na Mumbi Ngugi walisitisha utekelezaji wa usajili wa Huduma Namba hadi kanuni maalum ya kusimamia shughuli hiyo na itakayohakikisha kuwa data za wananchi ni salama, imewekwa.
Waliamua kuwa mfumo sheria iliyotumiwa kutekeleza usajili wa Huduma Namba haikuwa thabiti na huenda isihakikishe usalama wa data ya wananchi itakayokusanywa wakati wa usajili.