Serikali yaunda kamati kukabiliana na konokono
Na GEORGE MUNENE
SERIKALI imebuni kamati ya watu 15 ya kusaidia kupambana na mamilioni ya konokono ambao wamevamia mashamba ya mpunga ya Mwea katika Kaunti ya Kirinyaga na kutekeleza uharibifu mkubwa.
Konokono hao tayari wamesababisha uharibifu mkubwa katika ekari 34 za mashamba ya mpunga na wakulima wanahofia kwamba watamaliza mazao mashambani iwapo hawatanyunyiziwa kemikali ya kuwaua.
Kamati hiyo inaongoza na wanasayansi wataalamu Vincent Koskei na Raphael Wanjogu kutoka Bodi ya Kitaifa ya Unyunyiziaji wa Mashamba maji.
Kwa mujibu wa msimamizi wa mashamba ya Mwea Innocent Ariemba, kamati hiyo inalenga kuchunguza kemikali zilizopo madukani ili kubaini ile ambayo itatumika kuwaua konokono hao ambao hawana historia ya kuvamia mashamba Barani Afrika.
Aliongeza kwamba pia wanachunguza jinsi ambavyo konokono hao ambao kupatikana Amerika na bara Asia walifika nchini na kuvamia shamba hilo kubwa zaidi la mpunga Kenya.