Serikali yawataka wazee kula chakula bora
Na SAMMY WAWERU
Wazee wako katika hatari kuu kuambukizwa ugonjwa wa Covid-19 na wanapaswa kuwa waangalifu, imeonya Wizara ya Afya.
Waziri Msaidizi katika wizara Dkt Rashid Aman Jumanne amehimiza wazee kuzingatia lishe ili kuimarisha kinga yao ya mwili.
“Chakula faafu na chenye madini kamilifu kitiliwe maanani hasa kwa wazee,” Waziri akasema. Alipendekeza wazee wawe na uzoefu wa kula chakula chenye nguvu hususan nafaka zenye madini mengi ya wanga.
Ili kuimarisha kinga dhidi ya magonjwa hatari, Bw Aman alisema ni muhimu watu wale mboga na matunda kwa wingi, kwa kuwa ni mazao yaliyosheheni Vitamini.
Aidha, Waziri alisema visa vingi vya maambukizi na vifo miongoni mwa wazee vinahusishwa na magonjwa hatari kama vile ugonjwa wa Moyo, Figo na pia Kisukari.
“Ninahimiza wahudumu wa afya kufuatilia historia ya wazee hasa kuhusu magonjwa hatari,” alisema Dkt Aman.
Wakati huhuo, Wizara ya Afya Jumanne imetangaza maambukizi mapya 397 katika kipindi cha saa 24 zilizopita, wagonjwa 389 wakiwa ni Wakenya na 8 raia wa kigeni.
Maambukizi hayo yamebainika kutoka kwa sampuli 3,637, takwimu hiyo ikifikisha jumla ya visa 14,168 vya virusi vya corona nchini.
Wanaume wameendelea kuandikisha idadi ya juu ya maambukizi, ambapo Jumanne wamesajili visa 236 nao wanawake wakiwa 161. Mgonjwa wa umri mdogo ni mtoto wa mwaka mmoja, ule wa juu akiwa na miaka 90.
Katika kipindi cha saa 24 zilizopita, wagonjwa 642 wametangazwa kupona, idadi hiyo ikifikisha jumla ya 6,258 waliothibitishwa kupona kabisa nchini.
Watu 12 wamethibitishwa kufariki, idadi ya walioangamizwa na Covid-19 nchini ikifika 250.