Sh100,000 kwa atakayetoa habari kuhusu uharibifu na wizi wa miundombinu ya barabarani
Na MAGDALENE WANJA
MAMLAKA ya barabara za mijini – Kenya Urban Roads Authority (Kura) – imetoa kitita cha Sh100,000 kwa yeyote atakayetoa habari kuhusu uharibifu na wizi wa miundombinu ya barabarani.
Kulingana na Kura, wizi wa vifaa kama vile taa, vikingi na ishara za trafiki umeripotiwa kuwa wa juu zaidi katika siku za hivi punde.
“Mamlaka imetoa Sh100,000 kumkabidhi yeyote atakayetoa ripoti kuhusu wezi hao na washirika wao ili kufanikisha kukamatwa kwao,” ilisema taarifa hiyo iliyotiwa sahihi na kaimu mkurugenzi mkuu Bw Silas Kinoti.
Vilevile, mamlaka hiyo imetoa namba ambazo wananchi watazitumia kupiga ripoti kuhusu wizi wa vifaa hivyo.
Bw Kinoti alisema kuwa serikali inatumia Sh300 bilioni kila mwaka katika ujenzi wa barabara ili kufanikisha Ruwaza ya mwaka 2030.
“Kwa muda wa miezi mitatu, zaidi ya vikingi (poles) 30 vya stima vyenye thamani ya Sh2.5 milioni vmeibwa katika jiji la Nairobi,” akasema Bw Kinoti.
Kulingana na mamlaka hiyo, barabara zilizoathirika zaidi ni pamoja na Thika Superhighway, Outer Ring-Road, Ngong Road na Lang’ata Road.