Habari Mseto

Sh25m kwa aliyedungwa sindano ikamlemaza

September 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WANYORO

MWANAMKE aliyepata ulemavu kwa kutohudumiwa vyema baada ya kujifungua pacha katika hospitali moja ya Kanisa Katoliki katika Kaunti ya Meru, amepatiwa fidia ya Sh25 milioni na Mahakama Kuu ya Meru.

Jaji Alfred Mabeya aliamua kuwa wahudumu wa afya katika hospitali ya St John of God iliyo eneo la Tigania Mashariki walimlemaza Bi Lucy Kinya baada ya kumdunga dawa iliyomwathiri vibaya alipofika kuhudumiwa.

Bi Kinya, 30, alikuwa akifanya kazi katika hoteli moja.

Akitoa uamuzi huo, Jaji Mabeya alisema kuwa baada ya kuwasikiliza wataalamu wa afya na kutathmini ushahidi uliowasilishwa kwake, anaamini kuwa hospitali hiyo ndiyo ilimsababishia mlalamishi ulemavu huo.

Bi Kinya aliiambia mahakama kwamba alifika katika hospitali hiyo mnamo Juni 25, 2016, kujifungua pacha, ambapo akiwa katika chumba cha upasuaji, alidungwa mara nne mgongoni.

Alisema alipata fahamu baada ya muda wa saa tisa.

Alisema kuwa alipojaribu kuamka, alishindwa kutembea, huku miguu yake ikigeuka kuwa myeusi.

Alisema kuwa wahudumu walikataa kumwambia kilichokuwa kimejiri ambapo badala yake, walimweleza kwa madharau kwamba alikuwa akijifanya.