Sh81 miioni zilitumika visivyo katika kaunti 12 – Mhasibu Mkuu
Na GRACE GITAU
RIPOTI ya Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali imefichua kwamba kaunti 12 zilikosa kuwasilisha taarifa za kuthibitisha matumizi ya Sh81 bilioni zolizopokea kutoka kwa Wizara ya Fedha wakati uchaguzi mkuu wa 2017 ulipokuwa ukikaribia.
Hata hivyo, Mkaguzi Mkuu, Dkt Edward Ouko hakutoa wazo lake kuhusu majukumu ya kifedha yaliyotekelezwa na kaunti hizo mwaka wa kifedha wa 2016/17, hii ikiwa ina maana kwamba hakukuwa na stakabadhi za kushadidia matumizi ya fedha hizo.
Kulingana na ripoti hiyo, zaidi ya nusu za kaunti nchini zilikuwa katika hali mbaya ya kifedha mwaka wa kifedha uliokamilika Juni 2017, mwezi mmoja tu kabla ya uchaguzi mkuu kuandaliwa ambapo magavana wengi walishindwa kuvihifadhi viti vyao.
Ripoti hiyo pia inaonyesha tofauti kubwa katika hesabu za kifedha kati ya taarifa za kifedha zilizowasilishwa na kaunti mbalimbali na ile ya mtindo wa kisasa unaodhibiti kutumwa au kupokelewa kwa fedha za kaunti (IFMIS).
Taarifa hiyo ya Bw Ouko huenda inaashiria kwamba fedha hizo ziliporwa au zilitumika bila matumizi hayo kunakiliwa kwenye vitabu vya ukaguzi wa hesabu.
Kaunti zilizotajwa ni Nairobi, Nandi, Tana River, Vihiga, West Pokot, Bomet, Homabay, Kericho, Kitui, Lamu, Machakos na Migori.
Wakati uo huo, kaunti nyingine 12 zilionyesha mianya mikubwa katika Sh73 bilioni zilizopokezwa katika mwaka huo wa kifedha. Kaunti hizo zilikuwa Nyamira, Samburu, Kirinyaga, Murang’a, Tharaka Nithi, Kwale, Kisumu, Siaya, Turkana, Garissa, Isiolo na Embu.
Kulingana na ufichuzi huo, Kaunti ya Nairobi ilitumia vibaya Sh8 bilioni kati ya Sh10 bilioni zilizokusanywa kama kodi baada ya waziri wa fedha wa kaunti kukosa kuipeleka benkini namna inavyotakikana kisheria. Ripoti hiyo pia inafichua serikali ya Kaunti ya Nairobi ilikosa kusambaza Sh281 milioni kwa hospitali mbalimbali kama Pumwani na Mbagathi kugharamia kujifungua kwa akina mama bila malipo.