SHAIRI: Kwa nini tubaguane?
Na IZIRARE HAMADI
Uumbile lilo hariri, mola katuumbia,
Liwe shari au heri, adinasi jijazia,
Mapambo yake kahari, sote twayaajabia,
Kama sote umbile moja, tungejitambulisha.
Sote tuko kwa safari, hilo nawakumbushia,
Sangi zetu ni fahari, mola kutujaalia,
Humu ndani ya sayari, nini tunashindania,
Kama sote umbile moja, tungejitambulishaje?
Ukabila ni hatari, makabila hujitia,
Hiyo huwa ni dhahiri, macho wanaifumbia,
Nawaambia si siri, nchi yatuangushia,
Kama sote umbile moja, tungejitambulisha?
Ushakua utiriri, ukabila kuvalia,
Wenye dini na kafiri, wote waupalilia,
Hakika moyo ayari, umotoni waumia,
Kama sote umbile moja, tungejitambulisha?
Utu ushawa sufuri, sioni katu sharia,
Kwa laili wa nahari, wazidi kudidimia,
Lini taja siku nzuri, iwe siku ajnabia,
Kama sote umbile moja, tungejitambulisha?
Malenga:Izirare Hamadi
Eneo: Kisauni, Mombasa
Shule ya Upili ya Maweni