Habari Mseto

Shakahola: Watoto walinyongwa baada ya kushinda njaa, upasuaji wabaini

Na BRIAN OCHARO December 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

USHAHIDI mpya katika kesi kuhusu mauaji ya watoto Shakahola umeeleza kuwa, baadhi ya watoto waliwekwa njaa kwa muda mrefu kabla ya kunyongwa hadi kufa.

Maelezo hayo ya kusikitisha yalitolewa na daktari wa uchunguzi wa chanzo cha vifo wa serikali, Dkt Richard Njoroge, aliyeambia mahakama kuwa, kati ya watoto 191 waliokufa msituni, chanzo cha kifo cha watoto 42 hakikuweza kubainishwa.

Alisema sababu za vifo ziligawanywa katika makundi manane: sababu zisizobainika (miili 42), sababu zisizobainika kutokana na kuoza kwa kiwango kikubwa (miili 68), dalili zinazoendana na njaa (miili 42), njaa (miili 31), kukosa hewa pamoja na dalili za njaa (miili minne), kunyongwa kwa kubanwa shingo kwa mikono (mwili mmoja), jeraha la kichwa kutokana na pigo kali (mwili mmoja), na njaa pamoja na dalili za kukosa hewa (miili miwili).

Ilikuwa vigumu kubaini chanzo cha vifo kwa watoto wengi kwa sababu mabaki ya miili iliyopatikana yalikuwa mifupa mikavu au miili iliyooza kupita kiasi.

Kuhusu njaa iliyoambatana na dalili za kukosa hewa, Dkt Njoroge alieleza kuwa, miili hiyo ilionyesha dalili za upungufu wa oksijeni, ambao unaweza kusababishwa na kubanwa shingo kwa mikono, kuzibwa pua, magonjwa yanayoathiri mapafu, miongoni mwa sababu nyingine.

“Njaa ilitokea kwanza. Mtu alikuwa tayari anakufa kwa njaa kisha kukosa hewa kukafuata,” alisema.

Kuhusu jeraha la kichwa lililoambatana na njaa, alieleza kuwa miili hiyo ilionyesha majeraha ya pigo kali kwenye fuvu pamoja na dalili za njaa.

Daktari huyo aliwasilisha ripoti 191 za uchunguzi wa maiti kwa waathiriwa wote. Kesi ya mauaji dhidi ya mhubiri Paul Mackenzie na washukiwa wenzake itaendelea Januari 2026.

Bw Mackenzie na washukiwa wenzake 30 wameshtakiwa kwa mauaji ya watoto 191 yaliyotokea katika msitu wa Shakahola.

Watu zaidi ya 400 walifariki kwa kufuata mafundisho ya dhehebu lililowapotosha kufunga hadi kufa kwa madai kwamba wangeenda kukutana na Yesu.