• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 4:40 PM
Shambaboi achunguzwa kwa kudaiwa kumuua bosi wake

Shambaboi achunguzwa kwa kudaiwa kumuua bosi wake

Na TITUS OMINDE

MFANYIKAZI wa shambani ambaye ni mshukiwa mkuu katika mauaji ya mwajiri wake, mke wa aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Kakamega, Bw Paul Yatich alifikishwa mahakamani mjini Eldoret Jumatatu.

Boniface Kiptoo ambaye alikuwa akiishi na marehemu alitoweka mnamo Oktoba 15 punde tu baada ya Bi Loise Yatich Barisbet kuripotiwa kupotea.

Mshukiwa huyo amekuwa akisakwa na polisi na alikamatwa Oktoba 27 katika mtaa wa Umoja/Lanet mjini Nakuru.

Mpelelezi mkuu wa mauaji hayo, Bw John Wanyonyi aliambia Hakimu Mkuu wa Eldoret, Bw Charles Obulutsa kwamba mshukiwa alikamatwa akiwa na mali ya marehemu ambayo ilipotea baada ya mauaji yake.

Mshukiwa alipatikana na kadi ya ATM ya benki ya Equity,kadi ya Boresha Sacco pamoja na leseni ya udereva ambazo zilikuwa za marehemu.

Hata hivyo, upande wa mashtaka uliomba mahakama muda wa siku 14 ili kukamilisha uchunguzi wake kuhusiana na kesi hiyo kabla ya mshukiwa kusomewa mashtaka.

“Mheshimiwa, uchunguzi katika mauaji haya haujakamilika. Tunaomba mahakama itupe muda wa siku 14 kumzuilia mshukiwa ili tukamilishe kumhoji na kurekodi taarifa muhimu kutoka kwake,” Bw Wanyonyi alimueleza hakimu.

Vile vile, polisi walitaka kupewa muda wa kupeleka mshukiwa katika hospitali ya Rufaa ya Moi MTRH mjini Eldoret ili aweze kufanyiwa uchunguzi wa DNA.

“Ni bayana kwamba mshukiwa hajapinga maombi ya afisa mchunguzi katika kesi hii,hivyo basi mahakama imewapa polisi siku 14 kumzuilia ili kukamilisha uchunguzi wake kuhusiana na kesi hii,” alisema Bw Obulutsa.

Kesi hiyo itatajwa Novemba 12, mwaka huu..

Mwili wa marehemu ulipatikana katika chumba kimoja nyumbani mwake mnamo Oktoba 16 baada kuripotiwa kupotea.

Mshukiwa huyo ndiye mtu wa pekee ambaye alikuwa akiishi na marehemu baada ya kutengana na mume wake kwa takribani miaka 10 iliopita.

Washukiwa wengine wawili Laban Cheruiyot na Simon Lumile ambao walikamatwa wakiwa na gari liloibwa kutoka kwa marehemu katika eneo la Kabiyet kaunti ya Nandi wanatarajiwa kusomewa mashtaka leo Okotba 30.

Wakati huo huo wiki jana jamaa ya marehemu ilipokea agizo la mahakama kuzuia mume wa marehemu kuendelea na mazishi yake hadi pale washukiwa zaidi kuhusiana na mauaji hayo watakapo kamatwa.

You can share this post!

Askofu apendekeza shule za mseto pekee nchini

Savula na wake zake wakana kumumunya mamilioni ya serikali

adminleo