Habari Mseto

Sherehe ya mawakili ilivyoishia kwenye mauti ya mmoja wao

June 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

Na TITUS OMINDE

MAHAKAMA moja ya Eldoret imeelezwa jinsi karamu ya siku tatu iliyohusisha marafiki ilikumbwa na mauti baada ya wakili moja kumshambulia mwenzake kwa chupa ya pombe na kumuua.

Alhamisi, mwalimu mmoja wa shule ya msingi aliielezea mahakama hiyo matukio ya kabla ya wakili huyo kuuawa na mwenzake.

Bw Kelvin Odhiambo alieleza kuwa karamu hiyo ya ndani ya nyumba iliandaliwa na wakili fulani aliyealika marafiki zake 10, akiwemo wakili aliyeuawa Calvin Ngaira na mshukiwa Abel Mogaka ambaye pia ni wakili.

Mahakama iliambiwa kuwa Bw Mogaka, wakili anayehudumu Eldoret alimuua Ngaira mnamo Mei 18, 2019 baada ya wao kukosana katika karamu hiyo katika nyumba moja iliyoko eneo la Annex kando ya barabara ya Eldoret-Nakuru
Bw Ngaira, ambaye ni mtoto wa kiume wa kipekee katika familia yake, inadaiwa alikufa kutokana na majeraha, alipokuwa akitibiwa katika Hospitali ya Medi-Heal mjini Eldoret, alikokimbizwa na marafiki zake.

Mshukiwa ambaye alikana mashtaka ameachiliwa kwa dhamana ya Sh1 milioni na mdhamini wa kiasi sawa na hicho.

“Tulikuwa tukijifurahisha kwa kubugia aina mbalimbali za pombe na chakula kitamu tulichoandaliwa na mwenyeji wetu kwa siku nzima hadi usiku huku baadhi yetu tukitizama kandanda ya ligi ya Uingereza,” akasema Bw Odhiambo.

Mwalimu huyo wa shule moja ya kibinafsi mjini Eldoret, alikumbuka kuwa siku hiyo mwendo wa saa kumi na moja na nusu, marehemu Ngaira na mwanamke mmoja waliondoka nje wakifuatwa na Bw Mogaka aliyekuwa amebeba glasi ya pombe huku wenzake wakisalia chumbani.

“Muda mfupi baadaye nilisikia kilio cha mwanamke huyo kutoka nje na nikatoka nje kujua kile kilichokuwa kikiendelea. Lakini nikampata marehemu akiwa ameanguka damu ikivuja kutoka shingoni mwake,” akaeleza.

Alisema mshukiwa alikuwa amesimama mita chache nje ya nyumba hiyo.

Bw Odhiambo aliongeza kuwa aliona vigae vya glasi na chupa zilizovunjika katika eneo la tukio.

“Inashukiwa kuwa mwendazake alishambuliwa na kufa akiwa nje ya nyumba ya mwenyeji wetu aliyekuwa ametuandalia karamu ya siku tatu,” akaongeza Bw Odhiambo.

Aliambia jaji anayesikiza kesi hiyo kwamba hakumbuki ikiwa marehemu alidungwa na vipande vya glasi au chupa ya pombe kwani wote walikuwa walevi chakari kisa hicho kilipotokea.