• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
SHEREHE ZA SIKU YA WANAWAKE: Wito dhuluma dhidi ya wanawake nchini Kenya zitajwe janga la kitaifa

SHEREHE ZA SIKU YA WANAWAKE: Wito dhuluma dhidi ya wanawake nchini Kenya zitajwe janga la kitaifa

Na WAANDISHI WETU

VIONGOZI wa kike wameitaka serikali kutangaza dhuluma dhidi ya wanawake kuwa janga la kitaifa huku ulimwengu ukisherehekea Siku ya Wanawake.

Viongozi wanawake kutoka Kaunti ya Mombasa waliitaka serikali kutangaza hilo kufikia Machi 30.

Viongozi hao walioungana na makundi ya wanawake kuandamana walisema wamechoka, wana uchungu na kuchoshwa na habari za kila mara za wanawake kufa kwa njia zisizoeleweka.

Mwanamke apiga mayowe nje ya majengo ya Bunge wakati wa maandamano ya kupigania usawa wa kijinsia Machi 8, 2019, maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani. Picha/ Evans Habil

Katika Kaunti ya Mombasa, Mbunge wa Likoni Mishi Mboko alisema wanawake wanafaa kupewa nafasi sawa na wanaume.

“Tumetoka kwa thuluthi mbili, tunataka uwakilishi 50/50,” alisema Bi Mboko.

Wanawake waliitaka serikali kutokubalia viongozi wa kisiasa walioshutumiwa au waliohusishwa na dhuluma dhidi ya wanawake kuchukua wadhifa wowote wa uongozi, likiwemo baraza la mawaziri.

“Vyama vya kisiasa vinafaa kuwaadhibu wanachama wao wote walioshutumiwa au kuhusishwa na dhuluma dhidi ya wanawake kuambatana na Kifungu cha Sita cha Katiba,” alisema.

Jijini Nairobi, makundi ya wanawake jana yaliandamana mitaani kwa kile yalichosema ni ongezeko la mauaji ya wanawake.

Wanawake hao ambao walijumuika na Mwakilishi wa Kike wa Nairobi Bi Esther Passaris walikosoa jinsi serikali imekuwa ikikabiliana na dhuluma dhidi ya wanawake.

“Serikali imeonekana kulegea katika kesi za dhuluma dhidi ya wanawake. Kesi nyingi kama hizo huwa hazikamiliki vizuri. Zote huisha kwa hali isiyoeleweka,” alisema Christne Omao, mwanaharakati.

Rais kuingilia kati

Aliongeza kuwa ongezeko la visa vingi vya wanawake waliouawa na waume zao au watu tofauti linahofisha, na kuongeza kuwa serikali inafaa kuchukua hatua kabla ya hali hiyo kuzidi kwa viwango visivyoweza kukabiliwa, na kumtaka Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati.

Maandamano hayo yaliyoandaliwa na makundi ya wanaharakati kama vile Feminists in Kenya, National Government Affirmative Action Fund (Ngaaf), na Haki Africa, miongoni mwa mengine yalifanyika wakati ulimwengu uliadhimisha Siku ya kina mama, na yalifanyika pia Nairobi, Mombasa na Kisumu.

Jijini New York, wabunge wa Kenya walishutumiwa kwa kukataa kuheshimu Katiba na Mahakama ya Juu katika kuhakikisha usawa wa kijinsia katika Bunge la Kitaifa.

Shirika lisilo la serikali lililo na makao yake Amerika katika taarifa lilisema hayo saa kadhaa kabla ya ulimwengu kuadhimisha Siku ya Wanawake mnamo Ijumaa.

Kituo cha Carter Centre, ambacho husimamia uchaguzi kilichoanzishwa na aliyekuwa Rais wa Amerika Jimmy Carter kiliwataka wabunge kupitisha sheria kuhusiana na suala hilo kama inavyohitajika kikatiba.

Kituo hicho kiliitaka afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa kuhakikisha utekelezaji wa Kifungu 27 (8) cha Katiba.
Kifungu hicho kinasema hakuna jinsia moja inayofaa kuzidi thuluthi mbili katika uongozi katika taasisi za umma.

You can share this post!

BI TAIFA, JUMAMOSI, MACHI 9, 2019

NI KUBAYA! Arsenal iko pabaya Ligi ya Uropa

adminleo