SHERIA ZA MICHUKI: Zaidi ya watu 2,000 kizimbani kwa kukaidi sheria
Na RICHARD MUNGUTI
WASHUKIWA zaidi ya 2,000 walishtakiwa katika mahakama mbalimbali katika kaunti za Nairobi , Meru , Embu na Nyeri kwa kukaidi sheria za trafiki almaarufu Sheria za Michuki.
Maafisa wa polisi walitekeleza misako kuhakikisha wenye magari ya uchukuzi wa abiria wametekeleza sheria hizo.
Misako iliyofanywa ililenga kuhakikisha abiria wako salama na madereva na makanga wanahudumu na magari yaliyohitimu masharti yote yaliyotangazwa.
Tangu Jumatatu maafisa wa polisi walitekeleza misako kuwanasa waliokaidi sheria za Michuki kote nchini.
Wenye magari zaidi ya 500 walikamatwa katika misako iliyotekelezwa na maafisa wa Polisi wa kuhakisha sheria za trafik zimefuatwa kwa ukamilifu.
Wenye magari waliokaidi walikumbana na makali ya sheria. Sio tu magari ya uchukuzi wa abiria waliokamatwa peke yao mbali pia na wenye magari ya kibinafsi.
Waliofikishwa mahakamani walikabiliwa na mashtaka ya kukaidi sheria za trafik na kutozwa faini kulingana na makosa dhidi yao.
Katika kaunti ya Nairobi zaidi ya washukiwa 500 walifikishwa katika mahakama za Milimani na Makadara. Katika kaunti ya Nyeri zaidi ya washukiwa 300 walifunguliwa mashtaka katika mahakama mbali mbali wakidaiwa.
Kwa mujibu wa Polisi watu 188 walitiwa nguvuni Nyeri na magari 118 kukamatwa wakati wa msako uliotekelezwa.
Wenye pikipiki almaarufu boda boda wapatao 82 walinaswa wakati wa msako uliofanywa Jumatatu.Walifikishwa mahakanani jana.
Kamanda wa Polisi kaunti ya Nyeri Bw Ali Nuno aliambia wanahabari kuwa waliotiwa nguvuni hawakuwa wamejifunga mishipi na baadhi ya magari hayakuwa yamelipiwa bima.
Wenye boda boda hawakuwa wamevaa kofia pamoja na abiria wao.
“Ni lazima abiria wanaobebwa na boda boda wajue wanatakiwa kuvaa kofia na wanaoabiri magari ya uchukuzi wa umma lazima wafunge mishipi,” alisema Bw Nuno.
Bw Nuno alisema polisi hawatalengeza kamba hadi kila mmoja katika kaunti hiyo afuate sheria.
Kamishna katika kaunti hiyo Fredrick Shisia alisema mipango imefanywa na viongozi wa mashtaka wahakikishe kesi zilizopelewa mahakamani zimekamilishwa kwa haraka.
Katika kaunti ya Embu wenye magari 70 pamoja na wenye boda boda walishtakiwa kwa kukaidi sheria za trafiki. Madereva walioshtakiwa hawakuwa wamebandika picha zao inavyotakiwa.
Afisa mkuu wa polisi Embu West Julius Meli alisema wenye matatu ambazo hazikuwa zimetimiza matakwa ya kisheria kuondolewa kwenye barabara.
Katika mahakama ya Karatina waliofikishwa walitolewa faini kati ya Sh1,000 na Sh10,000. Washtakiwa walifikishwa mbele ya hakimu mkazi Bw Elvis Michieka.
Machifu na manaibu wao walishiriki katika msako wa magari mabovu kwenye barabara ya Karatina –Kiamariga katika kaunti ndogo ya Mathira Magharibi.
Katika kaunti ya Meru madereva 30 walitiwa nguvuni na kushtakiwa kwa makosa mbali mbali.
Madereva wengi walishtakiwa kwa kutokuwa leseni zinazosomeka kwa urahisi, kuendesha magari yasiyo na mikanda na matatu isiyo na msitari wa rangi ya jano.
Hakimu mkazi Bw Henry Miriti aliwaamuru madereva wa magari ya kibinasfi waliobeba abiria walipe faini ya Sh10,000 ama watumike kifungo cha miezi mitatu gerezani kwa Wanasiasa kadhaa kaunti ya Nyeri walijipata tabaani baada ya magari yao kuzuiliwa kwa kuvunja sheria.
Diwani maalum katika kaunti ya Nyeri Beth Nyawira alipelekwa kituo cha polisi kwa kuzua vurugu baada ya dereva wake na gari lake kukamatwa wakati wa msako huo na kuwekwa rumande.
Polisi walikataa kumsikiza duwani huyo wakisema lazima sheria itumike na dereva wake kushtakiwa pamoja na wengine. MCA wenzake walifika katika kituo cha polisi kumpa moyo Bi Nyawira.
Waliokamatwa Nairobi walishtakiwa katika mahakama za Milimani na Makadara. Washukiwa zaidi ya 300 walikamatwa katikati ya jiji la Nairobi na viunga vyake.
Waliokamatwa katika steji ya Kencom walitiwa pingu na kukalishwa chini ya miti iliyoko karibu wakisubiri kupelekwa mahakama ya Milimani Nairobi waliposhtakiwa.
Waliotiwa nguvuni walikuwa ni pamoja na madereva na makanga.
Madereva walishtakiwa kwa kutokuwa wameweka picha zao kwenye magari waliyokuwa wanaendesha. Walioendesha magari bila kuweka vithibiti mwendo pia hawakupona.
Na magari ambayo hayakuwa yamechorwa ule msitari wa majano yalikamatwa pia. Washtakiwa hao walishtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi katika mahakama ya Milimani Bw Ben Nzakyo.
Washtakiwa walikiri makosa na kutozwa viwango mbali mbali vya faini kati ya Sh500 na Sh10,0000. Washtakiwa walilipa faini zao kwa njia ya Mpesa na wengine wakalipa ndani ya mahakama.