Shirika la Groots Kenya lalaani vitendo vya ubakaji Kiambu
Na LAWRENCE ONGARO
WATU wanaopitia masaibu ya ubakaji wanastahili kupewa makao maalum ili kutengwa na wanaowadhulumu.
Mkurugenzi wa shirika la Groots Kenya, Bi Fridah Githuku, alisema kwa siku za hivi karibuni kumeshuhudiwa visa vingi vya ubakaji na ni bora serikali kuingilia kati ili kuwakinga waliodhulumiwa.
Alisema tayari shirika hilo linashirikiana na Kaunti ya Kiambu na benki ya Equity ili kujali maslahi ya wanawake.
Alisema lengo lao kuu ni kuona ya kwamba benki ya Equity inatoa mikopo kwa wanawake hasa wa mashinani ili kuendesha biashara zao huko.
“Wanawake ndio hutekeleza majukumu mengi katika jamii na kwa hivyo ni vyema kuyajali maslahi yao wakiwa maeneo ya mashinani,” alisema Bi Githuku.
Alisema pia wana ushirikiano wa karibu na wakfu wa MasterCard ili kuendelea kutetea maslahi ya wanawake.
Aliyasema hayo mnamo Ijumaa mjini Ruiru katika kongamano la wanawake kujadili maswala ya wasichana, wanawake, na hata wanaume kudhulumiwa katika jamii.
Kulingana na uchunguzi wa data iliyotolewa juzi, katika mwezi wa Aprili 2020 Kiambu ilikuwa ikiorodheshwa katika nafasi ya tatu kwa maswala ya dhuluma. Nairobi inaongoza ikifutiwa na Kisumu, huku Homa Bay ikiwa ya nne.
Naye mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Kiambu katika Bunge la Kitaifa Bi Gathoni wa Muchomba alitaka serikali ichukue hatua kali kwa wale wanaowanajisi wasichana wadogo.
Alipendekeza pia kuwa mtu yeyote ambaye aliwahi kupatikana na makosa ya ubakaji asipewe cheti cha tabia njema.
Alisema tayari amewasilisha mswada huo bungeni na anatarajia wabunge wenzake watamuunga mkono.
Alipendekeza kuwa mtu wa aina hiyo asipewe nafasi yoyote ya kazi serikalini.
Aliwashauri wanawake popote walipo wainuane badala ya masengenyo.
Alipendekekeza wasichana waliobebeshwa mimba wapewe makao maalum ili waweze kupata mazingira mema ya kulea watoto wao.
Alitoa changamoto kwa wanawake wapendane na kushirikiana wakati wa kugombea viti vya kisiasa.
“Sisi kama wanawake tuko na ushawishi mkubwa katika jamii na kwa hivyo tunastahili kuungana na kuleta mabadiliko muhimu katika jamii,” alisema Bi Muchomba.
Mbunge wa Gatundu Kaskazini Bi Wanjiku Kibe alisema eneo lake lina idadi kubwa ya wasichana wanaodhalilishwa kingono.
Alisema wiki mbili zilizopita, mwanamke mmoja alivamiwa kwake na watu kadha ambao walimbaka na kumuacha hoi.
Aliwashauri polisi wawe na utu wakati wanashughulikia kesi za ubakaji.
“Wasichana wengi wanaotendewa vitendo hivi vya kinyama hukosa kuripoti kesi hizo kwa sababu wao huulizwa maswala ambayo wanayaona ni ya aibu,” alisema Bi Kibe.
Alisema ataendelea kufuatilia kesi za ubakaji ambazo zinazidi kuripotiwa katika eneo lake la uwakilishi.