• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:55 PM
Shirika lataka wakuu wa madaktari wasukumwe jela kwa kugoma

Shirika lataka wakuu wa madaktari wasukumwe jela kwa kugoma

Na RICHARD MUNGTUTI

KITUO cha Sheria kinataka viongozi wa chama cha madaktari nchini (KMPDU) walioitisha mgomo ambao umeingia wiki ya tatu wafungwe jela kwa kutoufutilia mbali ilivyoagiza mahakama.

Shirika hilo linasema mgomo huo umesababishia Wakenya shida isiyo na kifani na kufanya wagonjwa kufariki kwa kukosa matibabu.

Kupitia wakili Dkt John Khaminwa, Kituo cha Sheria kimemsihi Jaji Bryan Ongaya awasukume jela Katibu Mkuu wa KMPDU Dkt Davji Atellah pamoja na mwenyekiti Dkt Abidan Mwachi na mweka hazina Dkt Mercy Nabwire.

Dkt Khaminwa amesema katika kesi aliyowasilisha chini ya sheria za dharura kwamba maafisa hao wakuu KMPDU walikaidi agizo la Mahakama kuu likiharamisha mgomo huo.

Wakili huyo mwenye tajiriba amesema “kitendo cha maafisa wakuu wa KMPDU kukaidi agizo la mahakama ni utovu wa hali ya juu na wanapasa kuchukuliwa hatua kali.”

Wakili huyo ameomba mahakama isisite kuwaadhibu maafisa hao kwa vile “maagizo ya mahakama yanapasa kutekelezwa jinsi yalivyo.”

Kituo cha sheria kimewashtaki Waziri wa Afya Bi Susan Nakumincha, KMPDU, Muungano wa Baraza la Magavana (CoG), Chama cha kitaifa cha Wauguzi (KNUN) na Mwanasheria Mkuu.

Wengine walioshtakiwa ni Waziri wa Masuala ya Leba na Tume ya Kushughulikia Mishahara ya Watumishi wa Umma (SRC).

Mnamo Machi 6 KMPDU kilitoa arifa ya mgomo kikilalamika kwamba serikali ilakataa kutekeleza makubaliano na maafikiano ya nyongeza ya mishahara na marupurupu mengine ya 2017.

Madaktari walianza mgomo na wameapa kuendelea nao hadi pale Serikali ikatakapotekeleza maafikiano kuhusu malipo na kuimarisha mazingira ya utenda kazi.

Kituo cha sheria kinasema kila mkenya yuko na haki ya kupata huduma za matibabu kwa mujibu wa Kifungu nambari 43 (1)(a) cha Katiba.

Lakini Jaji Ongaya mnamo Jumatano wiki hii aliipa Wizara ya Afya muda zaidi kufikia suluhu na chama hicho cha madaktari ndipo wanachama wao warudi kazini.

  • Tags

You can share this post!

NASAHA ZA RAMADHANI: Tukague nafsi zetu msimu huu wa mfungo...

Mama aliyekaribisha Gachagua kunywa chai kwa kibanda chake...

T L