Shoka la Jubilee lamwangukia Sankok
Na CHARLES WASONGA
JUBILEE imeendelea kuwaadhibu wabunge wandani wa Naibu Rais William Ruto huku uhasama ndani ya chama hicho tawala ukiendelea kutokota kila uchao.
Wa hivi punde kuangukiwa na shoka ni Mbunge Maalum David Ole Sankok ambaye ametimuliwa kutoka Kamati teule kuhusu Uwiano ya Kitaifa na Usawa ambako amehudumu tangu 2017 akiwakilisha Jubilee.
Kwenye taarifa kwa kikao cha bunge la alasiri Jumanne, Septemba 29, Spika Justin Muturi alisema alipokea barua kutoka kwa Kiranja wa Wengi Emmanuel Wangwe, akimjulisha chama cha Jubilee kimemfurusha mbunge huyo kama mwanachama wa kamati hiyo.
“Nimeridhika na utaratibu uliofuatwa na hatua hiyo imefikia mahitaji yote yaliyoko kwenye sheria za bunge nambari 176. Kwa hivyo, nimeidhinisha kuondolewa kwa mbunge huyo,” akasema Bw Muturi.
Kuondolewa kwa Bw Sankok kutoka kamati hiyo kumejiri miezi kadhaa baada ya Jubilee kutekeleza mabadiliko katika uongozi katika bunge la kitaifa na seneti na kamati za mabunge hayo, kwa kuwaondoa wabunge wandani wa Dkt Ruto.
Bw Sankok ni miongoni mwa kundi la wabunge wandani wa Naibu Rais, maarufu kama Tangatanga, ambao wiki jana waliandamana naye katika ziara ya kampeni katika kaunti ya Kajiado. Ni katika mkutano huo ambapo wabunge hao waliubua madai kuwa shughuli ya awamu ya pili ya usajili wa Huduma Namba itatumiwa kuiba kura mwaka wa 2022.
Kulingana na sheria za bunge chama chochote cha kisiasa kinaweza kuwaondoa wanachama wake kutoka kamati teule ya bunge, baada ya mwanachama huyo kupewa nafasi ya kujieleza.
Kiranja wa chama hicho kisha atamwandikia Spika,ambaye amepewa siku tatu baada ya kupokea waraka huo kumjulisha mbunge huyo anayeondolewa, kuhusu suala hilo.
Baada ya kutimuliwa kwa Sankok sasa bunge la kitaifa lina siku 14 kuteua mbunge mwingine atakayejaza nafasi hiyo.