• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Shughuli ya kukarabati barabara za mashinani yaendelea Zimmerman

Shughuli ya kukarabati barabara za mashinani yaendelea Zimmerman

Na SAMMY WAWERU

SERIKALI ya Kaunti ya Nairobi imeanza kukarabati upya baadhi ya barabara ambazo huwa hazipitiki msimu wa mvua eneo la Zimmerman.

Tayari ukarabati wa barabara ya Base na ambayo inaunganisha mtaa huo na Thika Super Highway umeanza.

“Hii ni mojawapo ya barabara kuu humu, msimu wa mvua haipitiki. Tunapania kuimarisha miundo msingi ili biashara ziimarike,” MCA wa Wadi ya Zimmerman Pius Mwaura aliambia Taifa Leo.

Hata ingawa hakueleza kiasi cha fedha zitakazotumika kufanikisha mpango huo, alisema itasaidia kumaliza msongamano kati ya barabara inayounganisha Roysambu na Zimmerman.

“Baadhi ya magari huhepa msongamano kwa kupitia Thika Super Highway, yanaingilia eneo la Carwash kuja Zimmerman. Ikikamilika, msongamano utapungua,” alisema Bw Mwaura.

Mwaka 2018 sehemu ya barabara ya Base ilikarabatiwa lakini shughuli hiyo ikasimamishwa.

Tayari shughuli ya umwagaji wa mawe na tingatinga kuyatandaza unaendelea.

Ufujaji wa mitaro ya majitaka eneo la Zimmerman ndio changamoto kuu, na ambao wakazi wanalaumu kuharibu barabara.

“Tunafurahia juhudi tunazoona, lakini pia serikali ishughulikie mitaro ya majitaka. Hufuja na maji yake machafu kusambaa barabarani,” anapendekeza mkazi.

 

  • Tags

You can share this post!

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Vikatizi vya mawasiliano bora na...

Waiguru sasa atangaza arusi rasmi

adminleo