Habari Mseto

Shule 50 zakosa matokeo ya KCSE

December 24th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na WAANDISHI WETU

WATAHINIWA wa Mtihani wa Kitaifa kwa Shule za Upili (KCSE) katika shule 50 watalazimika kusubiri hadi mwisho wa Januari mwaka ujao kujua hatima yao.

Hii ni baada ya Baraza la Mitihani ya Kitaifa Kenya (KNEC) kuzuilia matokeo yao.

Miongoni mwa shule zilizoathirika ni Shule ya Upili ya Kamotobo iliyo Kuria Mashariki, Shule ya Upili ya Wasichana ya Nyabisawa iliyo Suna Magharibi na Shule ya Upili ya Ageng’a iliyo Nyatike.

Zingine ni Shule ya Upili ya Emesa (Bomachoge Borabu) na Monianku (Gucha Kusini). Katika Shule ya Upili ya Mokubo iliyo Bomachoge Chache, mtahiniwa mmoja alikosa matokeo yake kwa kudaiwa kuiba mitihani.

Matokeo ya Shule ya Upili ya Wasichana ya Kapkenda iliyo Elgeyo-Marakwet pia yamezuiliwa na wanafunzi 226 wameathirika.

Maelfu ya watahiniwa wameathirika na hali hii huku shule husika zikinyamazia suala hilo kwa kuhofia kujiharibia sifa.

Wakati alipotangaza matokeo ya mtihani huo, Waziri wa Elimu, Bi Amina Mohamed alisema KNEC itatoa uamuzi baada ya kukamilisha upelelezi na kutoa ripoti yake Januari 31.

“Ninataka kuhakikishia taifa, watahiniwa walioathirika pamoja na wazazi wao kwamba haki itatendwa kuhakikisha hakuna mtahiniwa ataadhibiwa bila sababu,” alisema waziri.

Katika Shule ya Upili ya Ageng’a iliyo Kaunti ya Migori, wazazi na watahiniwa wenye ghadhabu waliivamia Jumamosi wakitaka kujulishwa matokeo yao lakini wakafukuzwa na mlinzi aliyekuwepo.

Baadhi ya watahiniwa na walimu wa Shule ya Upili ya Monianku wanakabiliwa na kesi za udanganyifu kwenye mtihani huo katika Mahakama ya Ogembo.

Shule ya Upili ya Wasichana ya Kapkenda ambayo imekuwa ikifanya vyema kwenye KCSE katika miaka iliyopita, lango lilifungwa tangu matokeo yalipotangazwa Ijumaa.

Juhudi za wazazi na wanafunzi kutaka kuingia jana ziligonga mwamba wakati mlinzi aliposisitiza aliagizwa asiruhusu mtu yeyote kuingia hadi wasimamizi wa shule waarifiwe kikamilifu kuhusu matokeo ya mtihani.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bi Jemima Sambai, alithibitisha kwamba watahiniwa hawajapokea matokeo yao.

“Sina habari zaidi kuhusu kinachoendelea kuhusu matokeo yetu. Tulipouliza maafisa wa Wizara ya Elimu mnamo Ijumaa, tuliambiwa tusubiri,” akasema.

Baadhi ya wazazi katika shule mbalimbali zilizoathirika walieleza matumaini yao kwamba suala hilo litatatuliwa.

Taarifa za Ouma Wanzala, Vivere Nandiemo, Magati Obebo na Titus Ominde