Habari MsetoSiasa

Si haki Tangatanga kuamriwa wakomeshe kampeni za 2022 – Ichung’wa

May 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MWANGI MUIRURI

MBUNGE wa Kikuyu, Kimani Ichung’wa sasa anamtaka Rais Uhuru Kenyatta afuate haki anapowataka wafuasi wa Tangatanga kukoma siasa za uchaguzi wa 2022.

Akiwa katika mahojiano na kituo cha redio cha Kameme amesema kuwa “rais huwa analenga tu wafuasi wa naibu wa Rais, William Ruto katika masharti ya kisiasa ilihali wale ambao hufuata mrengo wa siasa za “Kieleweke” huwa kila siku wako katika hafla za umma.

“Pia, wale ambao wanajitambulisha kama wakereketwa wa mrengo wa Hendisheki na ambao mara kwa mara huungana na mrengo wa Kieleweke huwa kiguu na njia wakipiga siasa lakini ikifika ni kukemewa, sisi wa Tangatanga ndio huzingatiwa,” akasema.

Bw Ichung’wa amesema kuwa “haiwezekani kamwe kuwe na vita kwa mfano, kati ya watu wawili, mmoja akubaliwe kumtandika makonde mwingine huku mwingine akiwa ameagizwa asithubutu kupigana.”

Amesema kuwa nia kuu ya mirengo ya Kieleweke na Hendisheki ni kumzima Ruto kuibuka mshindi 2022.

“Hapa hakuna haki yoyote na ndipo unapata mara kwa mara tukikaidi. Sisi tunarushiwa kila aina ya cheche katika kila aina ya majukwaa ya kisiasa na hapa tunaambiwa tumebanwa tusijihusishe na siasa.

“Huo si mpangilio wa haki kamwe na ikiwa kunaye anayefahamu haki ni nini, basi apige msasa matukio ya kisiasa hapa nchini na awe wa kujumuisha wote katika ushindani katika kukemea mikutano ya kisiasa,” akasema.

Bw Ichung’wa amesema kuwa kwa sasa Ruto anaonekana waziwazi kuwa ndiye ako guu mbele katika siasa za kuingia ikulu 2022, akionya kuwa “wale ambao hutegea tu kutuzwa mamlaka ya uongozi kupitia milango ya nyuma wangetaka kuzuke hali ya msukosuko kuhusu urithi huo ili katika hali ya utata itakayojiri, wasalimiwe tena na waitwe viongozi.”