Si miti tu, ukataji nyasi pia ni haramu, serikali yafafanua
Na VALENTINE OBARA
SERIKALI imefafanua kuwa marufuku dhidi ya ukataji miti ilijumuisha pia ukataji nyasi misituni na kuonya umma dhidi ya kuendeleza biashara hiyo.
Nyasi hizo wakati mwingi hutumiwa kwa mapambo kama vile kupandwa kando ya barabara za mijini na katika maboma ya watu hasa katika mitaa ya kifahari.
Kupitia kwa Shirika la Misitu la Kenya (KFS), serikali ilisema marufuku iliyotangazwa miezi michache iliyopita na Naibu Rais William Ruto dhidi ya kukata miti ilihitaji shughuli zote za uvunaji misituni zisitishwe isipokuwa upandaji miti pekee.
Mbali na miti na nyasi, bidhaa zingine zinazotokana na mimea ambazo hutafutwa sana misituni ni dawa za mitishamba.
“Uvunaji wa kitu chochote misituni ikiwemo nyasi katika misitu ya umma na ya kijamii umepigwa marufuku katika kipindi hiki. Mtu yeyote atakayepatikana akivuna bidhaa zozote katika misitu ya umma au ya kijamii atakamatwa na kushtakiwa mahakamani,” shirika hilo lilisema kwenye taarifa.
Mnamo Februari, Bw Ruto alitangaza marufuku ya ukataji miti kwa siku 90 katika misitu nchini ili kurekebisha hali mbaya ya hewa iliyosababishwa na ukataji wa miti kiholela.
Kipindi hicho cha marufuku kiliongezwa kwa miezi sita ilipofika Machi huku kukiwa na lengo la kupanda miche milioni 16.8 ifikapo mwaka wa 2022.
Wiki iliyopita, KFS ilisema ilipokea malalamishi kutoka kwa umma kuhusu watu wanaokata nyasi katika Msitu wa Aberdare.
Imebainika shirika hilo sasa linashirikiana na wadau wengine kuunda mwongozo ambao utasimamia ukataji, uuzaji na usafirishaji wa nyasi aina hiyo ili kuzuia uharibifu ambao umekuwa ukisababishwa na ukataji kiholela.
“Wauzaji na wasafirishaji wa nyasi hizi watahitajika kufuata kanuni zitakazokuwa kwenye mwongozo huo,” KFS ikasema.