Habari Mseto

SIKU 16 ZA HARAKATI: Shirikisho mojawapo la waumini wa Methodist lapinga dhuluma za kijinsia

December 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MAGDALENE WANJA

MAMIA ya wanawake ambao walikuwa wakihudhuria kongamano la kidini chini ya World Federation of Methodist and Uniting Church Women (WFMUCW) jijini Nairobi walifanya maandamano ya amani kuspinga unyanyasaji unaoelekezewa wasichana na wanawake.

Hii ni pamoja na kuadhimisha siku 16 za harakati dhidi ya dhuluma za kijinsia.

Ujumbe mkuu Alhamisi wiki jana ulikuwa ni kujitokeza na kuongea, ambapo waathiriwa wa visa vya dhuluma za kijinsia walishauriwa kunjitokeza na kuripoti kwenye vyombo vya usalama.

Wanawake hao walifanya maandamano hayo barabarani mbali na kongamano hilo lililokuwa likifanyika katika makao makuu ya kanisa la Methodist eneo la Kileleshwa.

Baadhi ya vijana wawakabidhi maua wanachama wa shirikisho la World Federation of Methodist and Uniting Church Women (WFMUCW) Novemba 28, 2019, Kileleshwa. Picha/ Magdalene Wanja

Waliongozwa na Rais wa shirikisho hilo Bi Sipwe Chisvo ambaye ni raia wa Zimbabwe.

“Usinyamaze iwapo unashuhudia visa vya dhuluma za kijinsia; hata kama wewe ni jirani, piga ripoti kwenye vyombo vya kisheria,” alisema Bi Chisvo.

Mratibu katika muungano wa WFMUCW, Bi Eunice Indangasi alisema kuwa tayari kanisa hilo limeanzisha vituo vya kuwaokoa waathiriwa wa dhuluma za kijinsia.

Wapo waliookolewa kutoka ndoa za mapema na ukeketaji.

“Pia tunawapa mafunzo walioathirika ili waweze kujitegemea baadaye maishani,” alisema Bi Indangasi.